You are currently viewing Benki ya Dunia yaahidi kuunga mkono maboresho zaidi bandari Dar

Benki ya Dunia yaahidi kuunga mkono maboresho zaidi bandari Dar

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Benki ya Dunia imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kusimamia vizuri wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi na maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam chini ya mpango  unaofadhiliwa na benki hiyo.

 Mpango huo unaojulikana kwa jina la Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP), awamu ya kwanza imekwisha na Benki ya Dunia imeahidi kujipanga kufadhili awamu ijayo.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia kanda ya Africa Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop (katikati) akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Bw. Plasduce Mbossa (kushoto) na Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar(watatu kulia) walipo tembelea bandari ya dar es salaam kujionea ufanisi na maboresho yaliyofanywa katika bandari hiyo.

Akizungumza leo Alhamisi jijini Dar es Salaam baada ya kikao kifupi na wajumbe wa TPA, Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshughulikia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, amesema maboresho yaliyofanywa mpaka sasa yanaakisi utendaji bora wa TPA.

“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika bandari hii. Tumeona idadi ya shehena inayoingia sasa imeongezeka. Hii ni kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Benki ya Dunia,” amesema Dkt Diop na kuongeza kwamba  umuhimu wa bandari hiyo ni mkubwa kwa sababu bandari inahudumia nchi sita zinazoizunguka Tanzania na ambazo hazina bandari.

Dkt. Diop ameahidi kuendelea kuishawishi Benki ya Dunia kuunga mkono awamu ya pili ya maboresho ya bandari hiyo ambayo yatajikita kwenye ujenzi wa gati nyingine na eneo la kuegeshea magari.

“Tunaamini maboresho hayo yanaenda kuboresha maisha ya Watanzania ambao watapata kazi katika mnyororo mzima wa thamani, pamoja na kuboresha maisha yao” amesema.

Ameongeza kuwa hii ni fursa kwa wawekezaji wakubwa na wadogo ambao watajenga viwanda vya bidhaa mbalimbali vitakavyokuwa na soko la ndani na nje ya nchi.

“Tanzania ina fursa nyingi hususani za kilimo, hivyo kupitia maboresho haya ya bandari yatasaidia vijana wengi wa Kitanzania kujiajiri na kuuza mazao yao nje ya nchi kwa kutumia bandari hii, na kupunguza tatizo la ajira nchini”, amesema Dkt Diop.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw Plasduce Mbossa,   amesema ujio wa Benki ya Dunia ni ishara ya wazi ya Tanzania ya kuwa na mahusiano mazuri na washirika mbalimbali wa maendeleo.

Benki ya Dunia walitoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania wa Dola za Marekani milioni 421na Serikali ya Tanzania iliongeza Dola milioni 64 za Marekani kwa ajili ya maboresho katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Maboresho haya yametusaidia kuweza kuteka soko la nchi zinazotuzunguka hasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Burundi, Rwanda na Zambia”, amesema Bw Mbossa.

Maboresho hayo yameifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo wa kupitisha shehena mara mbili ikilinganishwa na hapo awali.

Ripoti iliyopatikana inaonyesha kuwa kwa mwaka 2015/2016 bandari ilipitisha tani milioni 14, na mwaka huu ni tani milioni 33.