You are currently viewing Bunge lampongeza Dkt. Samia kwa uwekezaji sekta ya michezo

Bunge lampongeza Dkt. Samia kwa uwekezaji sekta ya michezo

Na Mwandishi Wetu Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limempongeza Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya michezo ambao umeendelea kuzaa matunda kupitia mafanikio ya timu mbalimbali za taifa katika mashindano ya kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 29, 2026 na wabunge mbalimbali wakati wakichangia baada ya Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya wakati kuwasilisha hoja bungeni kuhusu Azimio la Bunge la kuipongeza timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, kwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya AFCON 2026 inayoendelea nchini Morocco pamoja na kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la vijana chini ya umri huo mwaka 2026.

Akiwasilisha hoja hiyo, Bulaya alisema uwekezaji wa Dkt. Samia katika michezo umewezesha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika timu mbalimbali za taifa.

“Hivi tunavyozungumza, Serengeti Boys wameingia fainali na kufuzu Kombe la Dunia. Pia Tanzanite Queens (U-20) imefuzu kushiriki michuano ya dunia, huku Twiga Stars ikipewa nafasi ya kushiriki michuano ya wanawake Afrika (WAFCON),” alisema Bulaya.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge mbalimbali waliotumia nafasi hiyo kupongeza juhudi za Serikali katika kukuza michezo nchini pamoja na kuweka mazingira bora kwa vijana kuendeleza vipaji vyao.