Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa zaidi ya wanachama zaidi ya 20,000 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge na udiwani.
Taarifa hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, ambaye amesema jumla ya wanachama 4,109 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya ubunge katika majimbo yote 272 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Amesema kuwa kati ya waliochukua fomu hizo: 3,585 ni kutoka Tanzania Bara na 524 ni kutoka Zanzibar.
“Uchukuaji wa fomu umevunja rekodi, hamasa ni kubwa na habari ya mjini ni uchukuaji wa fomu ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Hii inaonesha zaidi kwamba CCM inaaminika, ni chama imara, kina sera nzuri, ndiyo matumaini ya Watanzania. Tumeona makundi mbalimbali yakichukua fomu-vijana, wanawake, watu wa kila rika, wasanii wameenda kuchukua fomu.
“Kwa takwimu waliochukua fomu kwa maana Bara na Zanzibar Ubunge na Uwakilishi ni 5,475 (Waliochukua fomu katika majimbo yote kwa Bara 3,585 Bara na Zanzibar ni 524). Udiwani katika Kata 3,960 bado taarifa zinakusanywa lakini kimsingi tunaweza kuwa na wagombea zaidi ya 15,000/= hivyo tunaweza kuwa na waliochukua fomu za udiwani na ubunge zaidi ya 20,000” amesema Makalla.
Makalla alisema zoezi hilo linaonesha hamasa kubwa ya kisiasa ndani ya chama, huku akisisitiza kuwa CCM itaendelea kufuata misingi ya haki, usawa na demokrasia katika mchakato mzima wa kupata wagombea wake rasmi.
“Hii inaonesha ni kwa kiasi gani wanachama wetu wamekuwa na imani kubwa na chama, na wako tayari kulihudumia taifa kupitia CCM,” alisema Makalla.
Kwa sasa, hatua inayofuata kuanzia tarehe 4 Julai, ni mchujo ndani ya chama ambapo wagombea watakaopitishwa wataingia kwenye kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Zoezi la uchukuaji wa fomu lilianza rasmi Tarehe 28, Juni na limehitimishwa jana Tarehe 2, Julai 2025 kwa maana watu kuchukua fomu Udiwani kwenye Kata na Wadi (kwa Zanzibar) Viti Maalum Wawakilishi na Viti Maalum Ubunge katika Majimbo na Ubunge.