Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Agosti 2, 2025 Tanzania itaingia kwenye rekodi ya kuwa moja kati ya nchi zilizowahi kuwa wenyeji wa fainali za Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Mchezo wa kwanza wa ufunguzi utafanyika Jumamosi ya wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itacheza dhidi ya Burkina-Faso.
Simba na Azam tayari zimeshatangaza kuwa zitatumia michuano ya CHAN – kusaka wachezaji, lakini pia zipo ambazo hazijatangaza, ila zitakuwa macho kumulika, pia fursa nyingine ni wachezaji wa Kitanzania kujitangaza ili kuweza kupata timu nje ya nchi.
Wamiliki wa mabasi na magari, mahoteli na vituo vya utalii pamoja na wafanyakazi kama vile madereva (bodaboda na bajaji) na wahudumu watafaidika kwa wageni watakaokuja kwa kutoa huduma mbalimbali.
Kwa ujumla wakati wa michuano ya CHAN, watu watakuwa na shughuli nyingi za kufanya ambapo kwa wafanyabiashara wenye tabia ya kujiongeza watapata pesa kiasi cha wao kutamani michuano hiyo iwepo kila mwaka nchini Tanzania.
Aidha ni muhimu watanzania hasa wafanyabiashara kuzichangamkia fursa za kibiashara zinazotokana na michuano hii.