Gavana wa Benki Kuu ya Comoro, Dk. Younoussa Imani jana Jumatano ametembelea makao makuu ya Benki ya CRDB na kumpa mwaliko Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela kuangalia uwezekano wa kuanza shughuli zake nchini humo.
Katika mazungumzo yao, Gavana Imani alimueleza Mkurugenzi Nsekela kuwa Comoro ina biashara kubwa na Tanzania na hiyo ni fursa kwa CRDB kuwa na operesheni zake nchini humo kwa faida ya pande zote.

Kwa upande wake, Nsekela alimueleza kuwa tayari CRDB ins operesheni nje ya Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Burundi na Comoro iko katika mipango yao na wataanza rasmi baada ya taratibu za ndani na upembuzi kukamilika.
Kikao hicho kilichoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro kilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Saidi Yakubu na Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Dk. El Badaoui Mohamed Ahmada.