Mabasi ya abiria, magari madogo, bajaji na pikipiki yameanza kupita katika baadhi ya maeneo ya barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT II) inayoanzia Kariakoo hadi Mbagala mara baada ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuratibu zoezi hilo kwa kipindi ambacho barabara hizo hazijaanza kutumika na mabasi yaendayo haraka.
Hali hiyo imeonekana leo mapema asubuhi tarehe 23 Oktoba 2024 ikiwa ni saa chache baada ya suala hilo kutolewa maelekezo ya kuwawezesha wananchi kutumia miundombinu ya mabasi mwendokasi iliyokamilika na haijaanza kutumiwa na mabasi hayo.
Bashungwa alitoa maagizo hayo ili kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam hususan majira ya asubuhi na jioni.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwa katika ziara yake ya usiku ya kukagua miradi ya maendeleo, alitoa maelekezo kwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) wa Dar es Salaam ifikapo saa mbili asubuhi magari madogo na mabasi ya abiria wawe wameanza kutumia barabara hizo mpaka mradi huo utakapoanza.