You are currently viewing DAWASA yaanza kufunga Pampu zitakazoimarisha huduma ya Maji

DAWASA yaanza kufunga Pampu zitakazoimarisha huduma ya Maji

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeanza rasmi zoezi la kufunga Pampu 3 kati ya Pampu 7 zilizowasili mapema Mwezi Mei Mwaka huu zinazotarajia kuimarisha na kupunguza changamoto za kihuduma katika Mikoa ya Dar es salaam na Pwani. 

Pampu hizo zitakazofungwa katika Mitambo mikubwa ya uzalishaji Maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini zina thaman ya Shilingi Bilioni 16.5 na zimeanza kufungwa kwa awamu kwa kuanzia katika Mtambo wa Ruvu Juu ulioko eneo la Mlandizi Mkoani Pwani.

Akizungumzia zoezi la ufungaji  wa Pampu hizo unaoendelea, Meneja wa Mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Juu, Mhandisi Juma Kasekwa amesema jumla ya Pampu tatu mpya zitafungwa mtamboni hapo na tayari wataalamu kutoka China wamefika ili kuhakikisha usimamizi sahihi wa ufungaji pampu hizo.

“Pampu zilizofika ni mahususi kwa kuchota maji ghafi kutoka mtoni na kuyasukuma katika mtambo wa kuyachakata/kusafisha maji, huku kuanza kufunga Pampu hizi ni ishara kubwa kwa Mamlaka kuwa sasa tunaenda kupunguza changamoto za kihuduma na kuimarisha huduma kwa kiwango kikubwa, Pampu hizi zitapunguza muda mwingi uliotumika zamani katika matengenezo ya Pampu za awali na zilizochangia kuwakosesha Wananchi huduma,” amesema Mhandisi Kasekwa.