You are currently viewing DC Bulembo aipongeza DAWASA kwa kutekeleza agizo la Majaliwa

DC Bulembo aipongeza DAWASA kwa kutekeleza agizo la Majaliwa

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kutekeleza kwa wakati agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kutatua changamoto ya ukosefu wa Majisafi kwenye Kata nne za Wilaya ya Kigamboni ili wananchi wanufaike na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa mradi mkubwa wa majisafi wa Kigamboni.

Bulembo ameeleza kuwa, Oktoba 16, 2024, Waziri Mkuu alitoa maagizo kwa DAWASA ya kuhakikisha Kata za Kisarawe II, Somangila, Kimbiji na Pembamnazi  wananchi wanafikiwa na huduma ya Majisafi.

Ameongeza kuwa jitihada kubwa za DAWASA zimeonekana ambapo kazi ya kulaza mabomba ya kusambaza maji sambamba na kutekeleza zoezi la kutambua wananchi wenye uhitaji wa maunganisho ya maji imekwisha kuanza.

“Hizi ni jitihada kubwa na za mfano za kurudi kwa Viongozi na kueleza hatua waliyoifikia katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu,” amesema.

Akielezea hatua iliyofikiwa, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa Mamlaka iliitikia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kutatua changamoto ya ukosefu wa majisafi kwenye Kata hizi nne, na kwamba kazi ya kufikisha maji ilishaanza na zoezi la kulaza mabomba ya kusambaza maji kwenye maeneo yaliyoelekezwa ya kihuduma inaendelea.

Ameongeza kuwa, mara baada ya kupokea maelekezo ya Waziri Mkuu, Mamlaka ilifanya tathmini ya kazi nzima na kubaini uhitaji wa ujenzi wa mtandao wa mabomba wa kilomita 221 ya kusambaza majisafi kwenye Kata zote nne, ambapo mpaka sasa jumla ya kilomita 160 za mabomba zimeshalazwa.

“kwa sasa tumebakiza  kilomita 60 za kukamilisha katika mwaka huu wa fedha ili wananchi waanze kupata Majisafi na salama,” ameeleza Mhandisi Bwire.

“Wito wetu kwa Wananchi wa maeneo haya ni kuwataka wajitokeze kwa wingi ili waweze kuunganishiwa huduma ya majisafi, kwa kuwa Serikali imeshawekeza fedha nyingi ili kila mwananchi apate huduma ya Majisafi,” ameeleza Mhandisi Bwire.

Mwakilishi wa Katibu wa CCM Wilaya ya Kigamboni Ndugu Hamza Halfan ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuitikia kilio cha wananchi wa maeneo haya na kutekeleza miradi hii ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa Majisafi. Hii ni hatua nzuri na ya mfano kwa sababu inalenga kutimiza ilani ya Chama ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 kwa wananchi wa mijini.

Naye mkazi wa mtaa wa Mwasonga Bi Hadija Omari ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kumtua ndoo ya maji kichwani kupitia mradi hii. “Jitihada hizi zimeleta faraja kubwa sana kwetu,” ameeleza.

Leave a Reply