Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo amezindua rasmi uhakiki, usajili na utoaji wa kadi za bima ya afya kwa wote wilayani humo ambapo katika awamu ya kwanza zaidi ya wananchi 11,021 wa kaya masikini wanatarajiwa kupatiwa bima hizo bure.
Hatua hiyo inalenga kutekeleza ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kampeni zake za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ambapo aliahidi kwamba ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa atahakikisha mpango huo wa bima ya afya kwa wote unaanza kutekelezwa.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kipeja – kata ya Kandawe – tarafa ya Itumbili – wilayani Magu, DC Lawuo amesema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanza kutoa kadi za bima ya afya kwa walengwa, ikiwemo wanufaika wa TASAF na wananchi wenye kipato duni.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila kizuizi cha kifedha, huku ikisaidia kaya masikini 2,493 kupata matibabu kwa urahisi wilayani humo.
“Hii ni awamu ya kwanza ila huduma hizi zinatolewa kwa kaya za watu sita kwa gharama ya Sh 150,000. Niwaombe wananchi wa Magu kutambua kuwa bahati haiji mara mbili, tuitumie fursa hii kwa sababu bima hizi zinapatikana kwa gharama nafuu sana ukilinganisha na matibabu yanayoenda kutolewa na bima hii ya afya.
Aidha, Mhasibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoa wa Mwanza, Francis Marwa amesema tangu zoezi hilo lianze tarehe 23 Februari mwaka huu wilayani Magu, wameshasajili kaya 250 zenye wanufaika zaidi ya 930 katika kata ya hiyo ya Kandawe.
“Zoezi hili linatukumbusha kwamba tunatakiwa kujikinga kabla ya kupata ajali kwa sababu sasa gharama za matibabu zinazidi kuwa kubwa, hivyo kwa wananchi wote watambue kuwa hii ni sheria ambayo imepitishwa mwaka 2023 kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya kabla ya kuugua,” amesema.
Ameongeza kuwa kadi hiyo inahusisha matibabu ya magonjwa 372 ambayo yanatibiwa bure bila usumbufu.
“Zoezi hili katika wilaya ya Magu ni la muda wa siku sita yaani hadi kufikia tarehe 28 Februari mwaka huu, hivyo tunawasisitiza wananchi wote walengwa wafike kwenye vituo vya usajili maana taarifa zinatolewa na watendaji wa vijiji na mitaa,” amesema.
Awali Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Magu, Eusebius Chanjali amesema amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Magu kuwa halmashauri imejipanga kutoa huduma za matibabu kwa ukamilifu ikiwamo utoaji wa dawa ambao umezidi kuimairika sambamba na huduma nyingine za uchunguzi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliopokea kadi hizo za bima ya afya kwa wote bure, Charles Kimoja na Juliana Motomkali wameishukuru Serikali kwa kuwapatia kadi hizo bure hasa ikizingatiwa kuwa sasa wanaweza kupata huduma bure za matibabu wao na familia zao.
Wamesema hapo awali walikuwa wakipata changamoto za matibabu kutokana na kutomudu gharama za matibabu hasa kunapotokea changamoto yoyote ya kiafya ndani ya familia zao lakini sasa hali itakuwa ni shwari.
