You are currently viewing DC Magu akabidhi baiskeli 67 kwa wakulima wa pamba

DC Magu akabidhi baiskeli 67 kwa wakulima wa pamba

MKUU wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari amegawa baiskeli 67 kwa wakulima viongozi wa zao la pamba kutoka tarafa za Kahangara na Itumbili wilayani humo ili kuwarahisisha usafiri wa kufika kwa wakulima wenzao na kuwaelimisha namna ya kulima zao hilo kwa ufanisi.

Nassari amegawa baiskeli hizo zilizotolewa Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza zao la pamba (CDTF) leo Jumatano katika Kijiji cha Ilungu wilayani Magu.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka wakulima hao kuzitumia baiskeli hizo kama chombo cha motisha katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuwawezesha wakulima wenzao kupata mavuno yenye tija.

“Usije kufunga siku hujafika hata kwenye shamba la mkulima kwa sababu ninyi mnaenda kuchukua jukumu linalofanywa na maofisa ugani ndio maana serikali ikaona iwatumie wahusika wenyewe ambao ndio ninyi wakulima. Kazi hii ya kuelimisha wakulima sio ya maofisa ugani pekee kwa sababu hawawezi kufika kila mahali, ndio maana kubwa ya kuwatumia ninyi kama tenashara wa pamba kwenye wilaya ya Magu,” amesema.

Naye Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Alphonce Awaki amesema wakulima hao viongozi watakuwa wanasaidia na maofisa ugani kusaidia.

Aidha, Diwani wa Kata ya Kandawe, Bomoa Lucas (CCM) amewataka wakulima hao viongozi kutumia baiskeli hizo kuwaelimisha wananchi waachane na kilimo cha mazoea ili waweze kupiga hatua kimaendeleo.

“Kwa sababu pamba hii inatuwezesha sisi madiwani kupata makusanyo ya kutosha ya halmashauri. Bila pamba kwa kweli hatuwezi… miaka ya nyuma watu walinunua ng’ombe, walioa wake wengi kutokana na kipato cha pamba.

Mmoja wa wakulima hao viongozi, Pius Mbogoma kutoka kijiji cha Mwamabanza, aliishukuru serikali kuwa kuwapatia vitendea kazi hivyo na kuahidi kwenda kuvitumia ipasavyo ili kubadilisha Maisha ya wakulima wenza.

“Tumefurahi sana… tunaiomba serikali iendelee kutuwezesha na sisi tutaendelea kushirikiana na mabwana na mabibi shamba,” amesema.

Leave a Reply