You are currently viewing Dk. Tulia aongoza kupitishwa kwa azimio jipya la UN

Dk. Tulia aongoza kupitishwa kwa azimio jipya la UN

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo terehe 25 Julai, 2025 ametangaza mafanikio makubwa katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kati ya Umoja wa Mataifa na Mabunge ya Kitaifa kupitia Azimio jipya lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN General Assembly), New York, Marekani.

Azimio hilo, lenye jina rasmi A/79/L.104 Interaction between the United Nations, National parliaments and the Inter-Parliamentary Union, liliwasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudhaminiwa na nchi zaidi ya 51 kabla ya kuwasilishwa rasmi kwa azimio hilo katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa na Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Dkt. Suleiman H. Suleiman.

Katika hotuba yake kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo, Mhe. Dkt. Tulia alisisitiza umuhimu wa kushirikisha mabunge kikamilifu katika kufanikisha Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030, kuimarisha amani na usalama wa kimataifa, na kusukuma mbele masuala ya usawa wa kijinsia, haki za binadamu na maendeleo jumuishi.

Azimio hilo linahimiza mambo mbalimbali ikiwemo Ushirikiano wa karibu kati ya UN na IPU katika masuala ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, afya, usawa wa kijinsia na teknolojia, Ushiriki wa wabunge katika mikutano mikuu ya UN, Ushirikiano na mashirika kama WHO, UNDP, na UN-Women katika kuimarisha uwezo wa mabunge kitaifa, Kuadhimisha Juni 30 kama Siku ya Kimataifa ya Mabunge na Septemba 15 kama Siku ya Demokrasia.

Kupitia azimio hili, Umoja wa Mataifa umetambua rasmi mchango wa IPU na mabunge ya kitaifa katika kusukuma mbele malengo ya kimataifa kwa njia shirikishi, ya kidemokrasia na yenye uwakilishi wa wananchi.

Hatua hii inadhihirisha nafasi ya Tanzania kama kinara wa diplomasia ya kibunge kimataifa na mchango wa moja kwa moja wa Mhe. Dkt. Tulia Ackson katika kuimarisha Taasisi za kibunge duniani.

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limepitisha azimio hilo kwa kura 153 za ndiyo na kura 1 ya hapana. Kufuatia hatua hiyo, Rais wa Baraza hilo Balozi Philemon Yang ameipongeza Tanzania kwa kurasimisha azimio husika. Adha, ameishukuru IPU kwa hatua zake za kuimarisha mahusiano na taasisi nyingine za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply