Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalumu), akisema ni kiongozi mzoefu na mwenye maarifa atakayemsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa mujibu wa Dkt Samia, ni mapema kufanya mabadiliko, lakini amechukua uamuzi huo ili kuendana na siasa za dunia zinavyokwenda ambazo zina jicho hasi na chanya kwa Tanzania.
Dkt Samia ameeleza hayo Jumamosi Januari 10,2026 wakati wa hafla ya kuipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na wanamichezo wengine wakiwemo wanariadhaa, mabondia na wana michezo mbalimbali iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Pale Ikulu nahitaji akili iliyopevuka, yenye maarifa mapana, uzoefu mkubwa na mtu ambaye yupo vizuri kwenye kujieleza na kueleza jambo litakaloeleweka.Nimepiga picha Serikalini, nikasema Profesa Kabudi atanifaa,” ameeleza Dkt Samia.
Januari 8, 2026, Dkt Samia alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri, akimpandisha Paul Makonda kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akichukua nafasi ya Profesa Kabudi aliyehamishiwa Ikulu.
