Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imechukua hatua ya kuwahamisha wananchi Ngorogoro kwa sababu eneo hilo lina baionuai nzuri kushinda mengine na fursa lukuki za utalii.
Sio hivyo tu, amesema ni Ngorongoro pekee ndilo eneo lenye vivutio vya kipekee vya utalii, ambavyo si rahisi kuvikuta katika maeneo mengine duniani, kadhalika ndani yake kuna madini muhimu yanayohitajika na wengi.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo, leo Alhamisi Machi 12, 2026, wakati wa hotuba yake, katika hafla ya kupokea taarifa ya Tume za Rais kuhusu mgogoro wa ardhi na uhamaji wa hiari, Ngorongoro.
Katika eneo hilo, kuna vivutio vingi ambavyo si rahisi kuvikuta katika eneo lingine na kuna ushahidi wa historia ya binadamu miaka milioni 3 iliyopita.
“Ni eneo muhimu kuhifadhiwa kwa faida ya Taifa letu, lakini faida na dunia. Ni eneo lenye misitu ya aina nyingi, pia kuna maeneo ya volkano ambazo baadhi zinaaminika kuwa ziko hai, kwa hiyo ni eneo la kuhifadhiwa na kunyenyekewa,” amesema.
