You are currently viewing Dkt. Samia alivyotumia siku 100 kubadili msingi wa elimu

Dkt. Samia alivyotumia siku 100 kubadili msingi wa elimu

Imechukua chini ya siku 100 kwa Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kukamilisha maandalizi na kuzindua mpango mkakati wa kisayansi kuhakikisha mwanafunzi anakuwa na umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, mkakati huo unalenga kuhakikisha mwanafunzi akifika darasa la tatu atakuwa na umahiri unaokubalika kimataifa wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mpango huo ni sehemu ya ahadi zilizotolewa na Dkt Samia wakati wa kampeni za urais, akiahidi kuzitekeleza ndani ya siku 100 za urais wake.

Utekelezwaji wa ahadi hiyo, umebainishwa Januari 31, 2026 na Profesa Mkenda, alipozungumzia utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Dkt Samia.

Amesema mkakati huo ulizinduliwa Januari 29, mwaka huu ili kumwezesha mtoto kuwa na msingi mzuri wa uelewa.

“Katika nchi yetu tuhakikishe kwamba ndani ya miaka nane, watoto wetu wawe na uwezo wa kusoma, kuhesabu na kuandika,” amesema.

Mpango huo, amesema unajumuisha mbinu za kufundisha hasa elimu ya awali watoto wajisikie kama wanacheza wakati huo huo wanajifunza, mafunzo endelevu ya walimu, nyenzo za kufundishia, kufanya tathmini na kushirikisha wazazi na walezi.

Ameeleza tayari Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), imeonyesha utayari wa kutoa Sh2 bilioni kwa ajili ya kusaidia mafunzo ya walimu.

Leave a Reply