Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika uzalishaji na uchakataji wa bidhaa za ndani, ikiwemo mchele, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika soko la Afrika.
Amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuimarisha miundombinu na kuunganisha Tanzania na mataifa jirani, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa bidhaa na kupanua masoko ya wazalishaji wa ndani.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo, Agosti 3, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkuu huyo wa nchi, ametoa mfano wa fursa zilizopo, amesema katika ziara zake nchini Ghana na Angola alibaini kuwa mchele wa Mbeya unafahamika na kuthaminiwa kutokana na ubora wake.
“Nilikwenda Ghana na Angola ndani ya Afrika. Nilishangazwa zaidi na Ghana walipokuwa wanazungumzia mchele wa Mbeya. Nikawauliza kwa nini mchele wa Mbeya, wakaniambia ukiupika nyumba nzima unanukia,” amesema.
Ameongeza kuwa viongozi na wafanyabiashara wa Ghana walieleza kuwa wanahitaji mchele huo kutoka Tanzania, lakini changamoto kubwa ni namna ya kuufikisha kwenye masoko hayo.
“Wakaniambia wanahitaji mchele wa Mbeya kutoka Tanzania. Tatizo letu ni connectivity ya kufikisha huko. Hiyo ndiyo kazi yenu sekta binafsi, mkae, mchemshe kichwa, tuone tunapelekaje bidhaa kwenye nchi jirani,” amesema.
Rais Samia amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya usafiri, ikiwemo Reli ya Kati na Reli ya TAZARA, ambayo itasaidia kuunganisha Tanzania na Angola kupitia Kapiri Mposhi hadi Bandari ya Lobito.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuondoa vikwazo vya usafirishaji wa bidhaa, huku akitoa wito wa kuongeza uzalishaji na uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ili Tanzania inufaike zaidi na fursa za soko la Afrika.
“Tunajitahidi kufanya connection, lakini sekta binafsi mkiweka misuli tutakwenda haraka zaidi. Tatizo ni connectivity, lakini bidhaa za kuuza tunazo. Tujitahidi kuzalisha kwa wingi na kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa,” amesema.
