Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kutumia ulimi wake kuzungumza ili kuzishawishi taasisi za fedha ndani na nje ya nchi, ziipatie fedha Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
Miongoni mwa taasisi alizozitaja ni Benki ya Dunia (WB), huku akiishuru kwa kufadhili miradi mbalimbali ukiwemo wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi Kiuchumi (HEET).
Kupitia mradi huo wa HEET, miundombinu ya vyuo vikuu mbalimbali nchini imeboreshwa, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikijenga Taasisi ya Sayansi za Bahari (UDSM-IMS) visiwani Zanzibar.

Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Januari 8, 2025 katika hotuba yake, wakati wa uzinduzi wa majengo ya IMS, Buyu visiwani Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo, amesema ataendelea kuzishawishi taasisi za fedha ndani na nje ya nchi, kuhakikisha zinashirikiana na Serikali ili kuiwezesha kifedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali.
“Tutajitahidi kutumia ndimi zetu kuwashawishi Benki ya Dunia na wadau wengine, watupatie fedha ili tukamilishe yale tuliyoyaanza,” amesema.
