You are currently viewing Dkt Samia: Poleni wafiwa, jeraha litatibiwa na sisi Watanzania

Dkt Samia: Poleni wafiwa, jeraha litatibiwa na sisi Watanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa familia zilizoondokewa na ndugu, jamaa na marafiki katika vurugu zilizotokea Oktoba 29,2025, akisema ni msiba wa watu wote.

“Damu ya Watanzania ni damu yetu sote, Mtanzania mmoja akiumia tumeumia sote, kuondokewa na Mtanzania mmoja tumeondokewa wote. Kwa hiyo tuwe pole wote,” amesema Dkt Samia.

Hii ni mara ya pili kwa Dkt Samia kutoa pole, mara kwanza ilikuwa wakati akihutubia na kulizindua Bunge la 13, mwezi uliopita jijini Dodoma.

Dkt Samia ametoa pole hiyo, leo Jumanne Disemba 2,2025 akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Amesema vurugu zilizotokea Oktoba 29 na kuendelea si desturi   wala utamaduni wa Watanzania, kila aliyeumia au kupoteza maisha ni Mtanzania mwenye haki sawa na wengine.

Amesema inatia uchungu kwa watu wachache walioratibu suala hilo (vurugu) ili Watanzania wawe kafara kwa malengo yao ya kisiasa yaliyojaa ubinafsi.

“Malengo yao ni tofauti na siasa iliyopo, lakini kwa sababu zozote hatukupaswa kuvuruga amani ya nchi yetu wala kusabbaisha vifo kwa watu wetu,” amesema Dkt Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt Samia amesema yaliyotokea yatatibiwa na Watanzania wenyewe, akisema hilo si la kwanza iliwahi kutokea mwaka 2001 na likatibiwa.

“Jeraha hili halitatibiwa na nje. Nje watatuwekea masharti watatufutia misaada…lakini watakaotibu jeraha hili ni sisi Watanzania,”

“Niwaombe tukae kwenye majukwaa yetu, wazee mna majukwaa yenu yana dini,makabila na vyama mbalimbali kaeni mzungumze, vijana wetu wasitumike, walivyotumika,”amesema.

Leave a Reply