Rais Samia Suluhu Hassan, amesema licha ya uhusiano mzuri wa kihistoria kati ya Tanzania na Namibia, bado kuna safari ya kuhakikisha hatua hiyo inaendana na kiwango cha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mataifa hayo.
Amesema ni ukweli usiopingika uhusiano wa Tanzania na Namibia katika uchumi bado mdogo akisema mwaka 2024 biashara kati ya mataifa hayo ilikuwa Sh 20 bilioni.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo Juni 20,2026 wakati akizungumza na wanahabari Ikulu Dar es Salaam, akiambatana na mgeni wake Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
“Kwa msingi huo, leo katika mazungumzo na Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah,tumekubaliana namna ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi na maeneo mengine ya kimkakati kama vile usalama wa chakula, uchumi wa buluuu, madini, mafuta na gesi,”
Rais Samia amesema amefurahishwa na hatua ya Rais Ndaitwah kuja Tanzania akiambatana na wafanyabiashara watakaoungana na wenzao wa Kitanzania ili kujadili mbinu bora ya kuimarisha biashara na uwekezaji.
“Nitumie fursa hii kuwahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia za biashara na uwekezaji zilizopo Namibia na wale Namibia kuja Tanzania kufanya hivyo,” ameeleza Dkt Samia.
