Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema dhamira ya Jeshi la Polisi ni kuwa karibu na wananchi na kiwe chombo kisichodharau kiashiria chochote cha hatari.
Rais Samia ameeleza hayo, leo Mei 28, 2026 wakati akihitimisha Mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, Kurasini, Dar es Salaam leo Mei 28, 2026.
Amebainisha kuwa hayo yote, yatafanikiwa endapo Jeshi la Polisi likiwa na mawasiliano ya karibu na vyombo vingine vya usalama katika kubadilishana taarifa za viashiria vya hatari.
“Wito wangu kwa Jeshi la Polisi ni kujenga imani kwa jamii ili kutimiza dhamira aliyoisema IGP Wambura kuwa,Jeshi la Polisi lina dhamira ya kuhakikisha linakuwa karibu na wananchi kubaini, kuzuia uhalifu kabla ya kutokea na kuhudumia wahanga kwa haraka zaidi, hili litawezekana kukiwa na ushirikiano wa karibu na wananchi na vyombo vingine vya usalama,” amesema.
Mkuu huyo wa nchi ameeleza kufurahishwa na mpango wa kuhusu maboresho ya mfumo, muundo na kisheria ya Jeshi la Polisi kama ilivyopendekezwa na Tume ya Haki Jinai.
