You are currently viewing Dkt Samia: Tutazihudumia  kikamilifu nchi zisizo na bahari

Dkt Samia: Tutazihudumia  kikamilifu nchi zisizo na bahari

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema uwekezaji wa Serikali katika mradi wa ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhi mafuta wenye thamani ya Sh 678.6 bilioni ni hatua ya kimakakati inayolenga kuimarisha Tanzania kama kitovu cha biashara cha ukanda na kimataifa.

Dkt. Samia ameeeleza hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa matenki hayo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.

Ujenzi huo ukikamilika utapunguza muda wa meli kusubiri kushusha mafuta kutoka siku 22 za sasa hadi siku saba tu, huku mchakato wa kushusha mafuta ukitarajiwa kufanyika ndani ya siku moja badala ya siku saba.

“Hatua hii ni uthibitisho kama Taifa tumeamua kujiandaa na kutumia kikamilifu jiografia ya nchi yetu kama lango kuu la kuhudumia nchi zisizo na bahari. Tumedhamilia kuhudumia wenzetu kibiashara na uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika ukanda huu,” amesema Dkt Samia.

Amesema bandari za Tanzania ikiwemo ya Dar es Salaam, zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi, ndio maana Serikali imeamua kufanya maboresho ya miundombinu na huduma za bandari za Bahari ya Hindi na maziwa makuu.

Dkt Samia amesema katika mchakato wanashirikiana na sekta binafsi kama ambavyo sera inavyoeleza kuwa ‘maendeleo yetu, hatutakwenda peke yetu, tutakwenda na sekta binafsi’.

“Tumekubaliana na kushirikisha sekta binafsi katika safari yetu ya maendeleo na tija ndio hii mnayoiona leo,” ameeleza Dkt Samia.

Leave a Reply