Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Jiji la Dar es Salaam, wasihodhi maeneo katika Soko la Kariakoo na kuwakodishia wafanyabiashara, badala yake shughuli hiyo ifanywe na Shirika la Masoko la Kariakoo.
Dkt Samia ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumapili Februari 8, 2026 alipozungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Soko la Kariakoo lililojengwa upya baada ya kuungua Juni mwaka 2021.
“Hapa nazungumza na wakubwa wa Jiji la Dar es Salaam, nisingependa kusikia ninyi wenyewe ndio mnahodhi maeneo mnakodisha watu. Shirika lenyewe la Masoko Kariakoo ndilo liwe linakodisha watu humu na ukodishaji uwe wa wazi na mapato yawe ya wazi,” amesema.
