Na Mwandishi Wetu | MCHUKUZI TV
Sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania inatarajiwa kupata msukumo mpya baada ya Shirika la Ndege la Flightlink kutangaza uzinduzi wa safari za moja kwa moja kati ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi kuanzia Julai 1, 2026.
Huduma hiyo mpya inatarajiwa kurahisisha safari kati ya Tanzania na Kenya kwa kuondoa hitaji la kupitia vituo vya kati, hatua itakayowanufaisha wafanyabiashara, watalii na wasafiri wanaotumia Nairobi kama kitovu cha kuunganisha safari za kimataifa.
Kwa mujibu wa Flightlink, njia hiyo ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma zake za kimataifa na kuongeza ufanisi wa usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Safari ya Kilimanjaro–Nairobi itakuwa njia ya tatu ya kimataifa kuendeshwa na shirika hilo baada ya huduma za Arusha–Wilson Airport nchini Kenya na safari zinazounganisha Zanzibar na Jomo Kenyatta International Airport.
Kwa upande wa utalii, huduma hiyo inatarajiwa kuongeza urahisi wa kufikia vivutio vya Kaskazini mwa Tanzania, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro, huku ikichochea ongezeko la watalii wanaoingia nchini kupitia Nairobi.
Aidha, wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Kenya wanatarajiwa kunufaika kwa kupunguza muda wa safari na kuongeza urahisi wa kufikia masoko ya kikanda.
Flightlink yenye makao makuu Dar es Salaam kwa sasa inaendesha safari katika miji mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar, pamoja na kutoa huduma za safari za kukodi ndege (charter) na usafiri wa dharura wa wagonjwa (Medevac).
Uzinduzi wa njia hii mpya unaonyesha hatua ya kuimarika kwa muunganiko wa usafiri wa anga ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kuongezeka kwa safari za moja kwa moja kunatarajiwa kuongeza ushindani katika sekta ya anga, kuimarisha biashara na utalii, pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji.
Wachambuzi wa sekta ya uchukuzi wanaona hatua hiyo kuwa ishara ya ukuaji wa mashirika ya ndege ya ndani na mwanzo wa upanuzi wa huduma za Flightlink katika masoko mengine ya kikanda.
MCHUKUZI TV – Connecting Tanzania’s Mobility
