Waziri wa Nishati, Dk. Juma Homera, ameitaka TANESCO kuongeza usimamizi kwa mkandarasi anayejenga njia za kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru na Tunduru hadi Masasi, ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuboresha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya kusini.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 214 kutoka Songea hadi Tunduru, pamoja na Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Tunduru. Sehemu ya pili ni ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 177 kutoka Tunduru hadi Masasi.
Homera ametoa agizo hilo Oktoba 25, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya kazi ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya nishati.
“Nimeona maendeleo ya mradi. TANESCO, msimamieni mkandarasi ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi. Dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wa mikoa ya kusini wananufaika na uwekezaji katika sekta ya umeme, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii,” amesema Homera.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Mhandisi Amos Kaihula, amesema utekelezaji wa mradi wa njia ya umeme kutoka Songea hadi Masasi umefikia asilimia 56, huku sehemu ya Tunduru hadi Masasi ikiwa imefikia asilimia 34.
Kaihula amesema TANESCO inaendelea kusimamia mkandarasi ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati na kwa ufanisi, akieleza kuwa miradi hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa mikoa ya kusini.
Miradi hiyo inatekelezwa na kampuni ya Kalpataru Projects International Limited ya India. Sehemu ya Songea hadi Tunduru inagharimu Sh bilioni 150.78, huku sehemu ya Tunduru hadi Masasi ikigharimu Sh bilioni 157.69. Kwa pamoja, gharama zake ni Sh bilioni 308.47.
Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuimarisha gridi ya Taifa na kuboresha huduma ya umeme kwa wananchi wa Ruvuma, Lindi na Mtwara, hatua inayoweza kusaidia shughuli za kiuchumi na kijamii katika mikoa hiyo.
