You are currently viewing IPTL kwafukuta, Mwanahisa ataka alipwe bil. 68.1

IPTL kwafukuta, Mwanahisa ataka alipwe bil. 68.1

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKATI hali ya ukimya ikiendelea kutanda katika kashfa maarufu ya Tegeta Escrow, kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imeingia katika mgogoro mwingine tena, safari hii ikiwa ni vita ya wanahisa wake huku mmoja akikimbilia mahakamani akiomba IPTL ifilisiwe ili kila mmoja apate kipande chake.

Kwa mujibu wa ombi lililofunguliwa katika mahakama kuu ya Dar es Salaam kama kesi ya madai namba 30802 ya mwaka 2024, kampuni ya Eurasia Holding Limited, ambayo ni moja kati ya wanahisa wa IPTL anayemiliki asilimia 10 ya hisa katika kampuni hiyo, anaiomba mahakama kutoa amri ya kufilisiwa kwa IPTL, au alipwe Dolla za Marekani Milioni 25,000,000 sawa na Shilingi Bilioni 68.1 ikiwa ni thamani ya hisa zake ndani ya IPTL.

Kwa mujibu wa ombi hilo ambalo limepangwa kuanza kutajwa tarehe 12 Februari 2025 saa tatu asubuhi mbele ya Jaji Mtembwa, kampuni ya Eurasia Holding Ltd, inalalamikia manyanyaso, mateso, kunyanyapaliwa, matumizi mabaya ya mali za IPTL na unyakuzi wa mali hizo bila kufuata utaratibu na uvunjifu mkuwa wa Malengo na Katiba ya Kampuni (Memorandum and Articles of Association) na sharia za nchi, inayofanywa na wanahisa wakubwa ndani ya IPTL, yaani PAN AFRICA POWER SOLUTIONS (T) LIMITED (PAP) and KARENGA PTY LTD pamoja na wakurugenzi wa IPTL. 

Kampuni hiyo inadai kwamba, kwa miaka mitatu sasa, haijawahi kupewa taarifa, wala kuitwa kuhudhuria kikao chochote cha IPTL, au hata kupewa taarifa za kiutendaji ndani ya kampuni hiyo, hivyo kuonyesha ni jinsi gani inavyo nyanyapaliwa na kutengwa katika shughuli zote za IPTL ambazo pia zinagusa maslahi yake kama mwanahisa, ikiwemo kufungua shauri mbalimbali mahakamani pamoja na maamuzi au makubaliano mazito yanayo fungamana na IPTL na kuathiri maslahi ya wanahisa wake, maamuzi/makubaliano ambayo Eurasia Holdings Ltd wanadai inafanywa mara kwa mara na wakurugenzi wa IPTL pamoja na wanahisa wakubwa bili kuwashirikisha.

Eurasia Holding Ltd inadai kwamba IPTL, japokuwa ni kampuni binafsi yenye wanahisa mbalimbali, inaendeshwa kama duka la mtu binafsi la kampuni ya PAP na KARENGA PTY LTD, akiendelea kudai kwamba kwa zaidi miaka 10 sasa, IPTL haijawahi kufanya mkutano wake mkuu wa wanahisa wote  kinyume na Katiba ya kampuni na kinyume na sharia ya makampuni ya Tanzania Sehemu ya 134 (1)(a), (b), (c), (d), (e) na (f)

Katika nyaraka hiyo ya mahakama, inadaiwa kwamba Bw. Harbinder Singh Sethi, ambaye ni mkurugenzi wa IPTL na pia Mkurugenzi Mtendaji wa makampuni yenye hisa nyingi ya PAP na Karenga PTY ltd, amekuwa anafanya maamuzi mazito peke yake kwa niaba ya IPTL kinyime na katiba ya kampuni hiyo na kinyume na sharia za makampuni ya Tanzania. 

Eurasia Holdings Ltd, wanadai kwenye nyaraka hiyo kwamba, tarehe 12 Juni 2023, Bw. Sethi, bila kushirikisha wanahisa wenzake, aligawa hisa za IPTL 150 kwa kampuni yake mpya ya Karenga PTY Ltd, hivyo kuifanya kampuni yake hiyo mpya kuwa mwanahisa mkubwa zaidi ndani ya IPTL, kinyume na Katiba ya kampuni na sharia ya makampuni ya Tanzani.

Kwa mujibu wa Eurasia Holding Ltd, kitendo cha Karenga PTY Ltd kumiliki hizo hisa 150 ndani ya IPTL kinyemela bila kupewa taarifa, inaathiri haki zake na pia inaonyesha ni jinsi gani inavyonyanyaswa na kunyanyapaliwa akiwa ni mwanahisa mwenye hisa chache ndani ya IPTL. 

Inadaiwa pia kwamba tarehe 01 Machi 2021, bila taarifa wala kupata idhini ya wanahisa wote wa IPTL, Bw. Sethi akidai anaiwakilisha IPTL na PAP, peke yake, aliingia katika makubaliano na serikali ya Tanzania (Deed of Settlement) katika shauri namba 90 ya mwaka 2018 katika mahakama kuu Dar es Salaam, ambalo ilipelekea kutolewa amri (Consent Decree) ya tarehe 19 Machi 2021. 

“Hatua ya kuingia katika makubaliano hayo, Bw. Sethi alifanya mlalamikiwa (IPTL) kulipa kiasi kikubwa cha fedha kisichokubalika, kama malipo ya madai yasiyo ya msingi ambayo inajumuisha madai katika hukumu ya kesi iliyofanyika katika mahakama za kigeni ambazo bado hazijakubalika katika mahakama za Tanzania. 

Pia aliweka rehani madai yote halali za IPTL yatokanayo na mkataba wa kufua na kuuza umeme kati yake na TANESCO na kukubali kusitishwa kwa mkataba huo na kuiondolea TANESCO majukumu na madai yatokanayo na mkataba wa kuuziana umeme ,” inasomeka sehemu ya nyaraka hiyo.  

Eurasia Holding Ltd wanadai kwamba nyaraka za makubaliano hayo na Serikali yalisainiwa kwa niaba ya IPTL na mwanasheria wa Bw. Sethi, anayeitwa Omar Iddi Omar na kaka yake Bw. Sethi anaitwa Manjit Singh Sethi, bila maazimio ya bodi ya wakurugenzi wa IPTL iliyompa mamlaka Bw. Sethi kufanya mazungumuzo katika shauri namba 90 ya mwaka 2018 kwa kuiumiza IPTL kama alivyofanya, na mbaya zaidi, kuwaruhusu wakili wake na kaka yake, ambao hawakuwa na mamlaka ya kusaini nyaraka yoyote kwa niaba ya IPTL, kufanya mazungumuzo na kusaini nyaraka nyeti kwa niaba ya IPTL.     

Inadaiwa kwamba kwa njia ya makubaliano hayo na amri iliyotolewa, mwanahisa mkubwa huyo anaifilisi kampuni ya IPTL kinyume na utaratibu bila kumshirikisha mwenye hisa chache (Eurasia Holdings Ltd), hivyo kuitumia vibaya mali zilizowekezwa ndani ya kampuni na kujinyakulia mali hizo kinyemela kinyume na Katiba ya IPTL na sharia za nchi sehemu ya 28(2) ya sharia ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2019. 

Pia inadaiwa kwamba utekelezaji wa amri yatokanayo na makubaliano hayo, itainyima Eurasia Holdings Ltd haki yake ya zaidi ya Dolla za Marekani milioni ishirini na tano (US$ 25m) ikiwa ni thamani ya uwekezaji wake, mali na haki zingine zinazotokana na asilimia 10 (10%) za hisa zake ndani ya IPTL.

Eurasia Holding Ltd inadai kwamba IPTL, ikishawishiwa na wanahisa wakubwa (PAP na Karenga PTY Ltd) zinazomilikiwa na kuendeshwa na Bw. Sethi, imefungua shauri namba 14259 ya mwaka 2024 katika mahakama dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wizara ya Nishati, bila kushirikisha Eurasia Holdings Ltd kama mwanahisa wa IPTL.

Nyaraka hiyo ya mahakama pia inadai kwamba tarehe 28 Novemba 2023, Mkurugenzi wa IPTL anayeitwa James Basil Yarah, akijifanya ni Mkurugenzi wa Eurasia Holding Ltd aligushi maazimio ya bodi ya Wakurugenzi wa Eurasia Holding Ltd, akiitumia nyaraka hiyo ya kugushi kwa maelekezo ya Bw. Sethi, akafungua shauri namba 917/01 ya mwaka 2023 katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania Dar es Salaam dhidi ya Serikali ya Tanzani.     

Eurasia Holding Ltd anazidi kudai kwamba kuna hali mbaya ya kutokuelewana kati yake na mwenye hisa nyingi, kuhusu umiliki na uendeshaji wa shughuli zote za IPTL, hali iliyopelekea hata baadhi ya wakurugenzi wa IPTL na baadhi ya wanahisa kuto kuzungumuza kabisa. 

Eurasia Holdings Ltd inadai katika ombi lake kwamba hali iliyofikia ndani ya IPTL, haina njia nyingine ya kutafuta ufumbuzi tofauti na kuiomba mahakama itoe amri ya kufilisiwa kwa IPTL kwa mujibu wa kifungu cha 275, 279(1)(e) na 281(1) ya Seria ya Makapuni, Sehemu ya 212 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Leave a Reply