You are currently viewing Kamati ya uchumi yapongeza zoezi la upimaji shirikishi Magu

Kamati ya uchumi yapongeza zoezi la upimaji shirikishi Magu

Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri imetembelea Kijiji cha Matela kata ya  Nyanguge  kukagua maendeleo ya zoezi la upangaji na upimaji shirikishi wa ardhi linaloendelea kutekelezwa na Halmashauri kwa lengo la kuweka mpangilio bora wa matumizi ya ardhi, kurasimisha makazi na kuimarisha mipango ya maendeleo ya maeneo ya makazi.

Ziara hiyo ililenga kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa zoezi hilo, kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu pamoja na kubaini changamoto zinazojitokeza ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Mh.Herbert Faustine  amepongeza wataalamu wa Idara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia zoezi hilo, akieleza kuwa upangaji na upimaji wa ardhi ni msingi muhimu kwa maendeleo endelevu ya Halmashauri.

Amesema zoezi hilo litasaidia kuondoa migogoro ya ardhi, kuwezesha utoaji wa hati za umiliki, kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na utoaji wa huduma za kijamii.

Pamoja na pongezi hizo, Mwenyekiti aliitaka Halmashauri kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya madalali wa ardhi wanaojitokeza baada ya maeneo kupangwa na kupimwa.

Alieleza kuwa baadhi ya madalali wamekuwa wakichochea migogoro na malalamiko kwa wananchi kupitia uuzaji usiofuata taratibu au upotoshaji wa taarifa kuhusu umiliki wa viwanja.

Amesisitiza kuwa Halmashauri iendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu sahihi za umiliki na uhamishaji wa viwanja pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kujihusisha na udalali usiofuata sheria.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo mbele ya Kamati, Afisa maendeleo ya Ardhi  wa Halmashauri, Bi. Yuster Byabusha amesema hadi sasa jumla ya vipande vya ardhi 1,253 vimepangwa na kupimwa katika kijiji chenye vitongoji vitano, huku zoezi likiendelea kwa mujibu wa mpango uliowekwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Mh. Edward Kihamba alizitaka idara ya ardhi na wataalamu wanaosimamia zoezi la upangaji na upimaji kuhakikisha wanawawezesha wananchi kukamilisha taratibu zote za kupata hati za umiliki wa ardhi mara baada ya upimaji kukamilika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji  wa Halmashauri, Mohamed Ramadhani  amesema zoezi la upangaji na upimaji shirikishi ni endelevu na ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri wa kuhakikisha maeneo ya makazi yanapangwa kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi na mahitaji ya maendeleo ya baadaye.