Serikali imesema uamuzi wake wa kusitisha kwa muda utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa umetokana na sababu za kiusalama baada ya kubainika viashiria, dalili na uthibitisho wa matishio ya amani nchini.
Akizungumza na BBC Swahili, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema zuio hilo si la kudumu bali ni la muda, likilenga kutoa nafasi kwa vyombo vya usalama kushughulikia tishio lililopo.
Amesema hali itakapotengemaa na tathmini za usalama kuridhisha, shughuli zitaendelea kama kawaida kwa mujibu wa sheria.
Katambi, amesema Serikali imefanya uamuzi huo kwa kutumia uzoefu wa matukio ya Oktoba 29, 2025 yaliyosababisha vifo vya wananchi, uharibifu wa mali na kuvuruga shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali.
Amesema baada ya matukio hayo, vyombo vya usalama vililaumiwa kwa kutokuchukua hatua mapema licha ya kuwepo kwa viashiria vya hatari.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imeamua kutodharau taarifa yoyote ya kiusalama na kuchukua hatua za tahadhari kabla ya madhara kutokea.
Amesisitiza lengo ni kulinda maisha ya wananchi, mali zao na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye utulivu.
