Rais mstaafu wa Tanzania, Dkt Jakaya Kikwete amemtaja Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa mama mwema, anayejali changamoto za wananchi na mwepesi wa kuchukua hatua.
Katika kauli yake hiyo, Dkt Kikwete amesema kiongozi huyo amezikabili changamoto zote za wananchi wa Mkoa wa Pwani na mikoa mingine ya Tanzania kwa mafanikio, ufanisi, umakini na ujasiri.
Dkt Kikwete ameyasema hayo, leo Jumapili Septemba 28, 2025 alipozungumza katika mkutano wa kampeni za urais, uliofanyika wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.

“(Dkt Samia) umeiongoza nchi yetu vizuri, wewe ni mama mwema unajali changamoto za wananchi unaowaongoza na mwepesi wa kuchukua hatua,” amesema.
Katika hotuba hiyo, Dkt Kikwete amesema Dkt Samia amezikabili changamoto zinazowakabili wananchi wa Pwani kwa mafanikio, ufanisi, umakini na ujasiri.
“Umetutendea mema mengi, umetutengea mazuri mengi, ni wajibu wetu sasa kukulipa mema, tutakulipa kwa mema uliyotutendea, tutajaza kura kwa wingi hadi zifurike kwenye sanduku la kura za mgombea urais,” amesema.
Amesema anatambua umuhimu wa kumwezesha afanye kazi kwa ufanisi kwa kumpatia wabunge na madiwani wa CCM.
“Tunakuhakikishia kama bunge linalomalizika sasa, wabunge wote wa CCM na litakalokuja kutoka Pwani wabunge wote wa CCM na naamini nchi nzima itakuwa hivyo.
“Hatuko tayari mheshimiwa Rais na mgombea wetu, kuchanganya pumba na mchele. Tunayajua madhara yake na hatutathubutu kufanya hivyo,” amesema.
Ameeleza furaha yake na kinachomtia moyo zaidi ni kumwona Dkt Samia akiwa na afya na nguvu za kutosha, licha ya kuchanja mbuga katika mikoa mbalimbali, tangu alipoanza kampeni za urais.
