Wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda wametia saini nakala ya awali ya mkataba wa amani baina ya nchi hizo mbili mjini Washington.
Hayo yameelezwa kwenye taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari iliyotolewa nchi hizo mbili na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani.
Taarifa hiyo imesema mkataba huo unajumuisha vipengele vya kuheshimiwa kwa hadhi ya mipaka ya kila upande, kukomesha uhasama, kuweka chini silaha na kujumuishwa kwa makundi ya waasi ndani ya mifumo ya dola.
Pia pande hizo mbili zimeahidi kufanya mkutano wa ngazi ya mawaziri wiki inayokuja na zimewaalika viongozi wa pande zote mbili kuhudhuria.
Kutiwa saini mkataba huo kunaweza kufungua njia ya kumalizika kwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu mashariki mwa Kongo ambako jeshi la serikali linapambana na kundi la waasi wa M23 inalosema linaungwa mkono na Rwanda.
Marekani ilijitwika jukumu la upatanishi baada ya juhudi za kikanda kushindwa kuumaliza mzozo huo. Qatar pia ilizikutanisha pande hizo mbili mwezi Aprili kwa mazungumzo ambayo hayakuzaa matunda