Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka minne gerezani, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kwa kosa la uchochezi.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Ijumaa Novemba 6, 2026 na Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Dustan Ndunguru.
Awali, kiongozi huyo wa upinzani alishitakiwa kwa kosa la uhaini na Mahakama imemkuta na kosa dogo la uchochezi na ndilo alilohukumiwa nalo. Mahakama pia imemweleza kuwa ana haki ya kukata rufaa.
Awali, akizungumza kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Lissu alisisitiza kuwa haombi msamaha kwa sababu anaamini hana hatia. Alipinga kutiwa hatiani kwa uchochezi, akisema shtaka alilokuwa akikabiliwa nalo lilikuwa la uhaini.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Baadaye alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 10, 2025, ambako alisomewa shtaka la uhaini.
Hadi leo, amekuwa kizuizini kwa takribani mwaka mmoja na miezi saba akisubiri kukamilika kwa kesi yake. Akizungumza mahakamani kabla ya kupewa adhabu, Lissu amesema leo ni siku yake ya 577 akiwa mahabusu.
