Mamlaka katika jimbo la Kerala kusini mwa India wametoa tahadhari baada ya meli iliyokuwa imebeba mafuta kuzama katika bahari ya Arabia.
Taarifa ya jeshi la wanamaji la India imefahamisha kwamba mabaharia wote 24 waliokuwamo kwenye meli hiyo wameokolewa.
Jeshi hilo limesema meli hiyo kwa jina MSC ELSA 3 ilikuwa inasafiri kutoka bandari ya India ya Vizhinjam kuelekea Kochi ilipata hitilafu siku ya Jumamosi na kuwasiliana nao.
Wizara ya Ulinzi ya India ilithibitisha kuokolewa kwa mabaharia hao 24 ambao wengi wao wanadaiwa kutokea Georgia, Urusi, Ukraine na Ufilipino.
Kontaina 640 zilikuwepo katika meli hiyo, ikiwemo 13 zilizoandikwa mzigo hatari na 12 zikiwa na madini ya Calcium carbide. Hakuna taarifa zozote hadi sasa kuhusu mzigo uliokuwa ndani ya makonteina hatari.