You are currently viewing Mageuzi ya Rais Samia yachochea uandishi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria

Mageuzi ya Rais Samia yachochea uandishi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema Kitabu cha “Falsafa ya Sheria ya Mama Samia” kilichoandaliwa kinaakisi utawala wa sheria wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema utawala wa sheria huo unaojumuisha mazingira ya maridhiano na uwekezaji, uwazi, huduma, haki na maendeleo ya wananchi.

Ameyasema hayo leo Julai 10, 2026, jijini Dar es Salaam na kueleza wazo la kukiandika  llitokana na tafakari ya kina kuhusu uelekezo mzima wa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema walijiuliza katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia  ilitumika kwa namna gani kuleta mageuzi?

Amesema wamejiuliza pia kama kuna mantiki inayounganisha marekebisho ya sheria au mabadiliko ya sera, maboresho ya taasisi na matokeo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema je mambo hayo kama wanaweza kuyaeza kwa ushahidi kwamba sheria imeanza kutumika zaidi kama chombo cha maendeleo na siyo chombo cha udhibiti.

“Maswali hayo ndio yaliyozaa wazo la ’Falsafa ya sheria ya Mama Samia’. Tuliona katika Awamu ya Sita kuna mwelekeo unaojitokeza wazi yani bayana kutumia sheria, sera, taasisi na mifumo ya utekelezaji kujenga mazingira ya maridhiano na uwekezaji, uwazi, huduma, haki na maendeleo ya wananchi,”  amesisitiza.

Aidha, amesema  kitabu hicho kinatarajiwa kuwa rejea muhimu katika uchambuzi wa sera na sheria, huku kikitoa nafasi kwa wasomi na wataalamu kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha mfumo wa sheria na maendeleo ya Taifa.