You are currently viewing Magu yatoa mikopo ya milioni 330 kwa vikundi 28

Magu yatoa mikopo ya milioni 330 kwa vikundi 28

KATIKA kuwawezesha wananchi kiuchumi, Halmashauri ya Wilaya ya Magu imetoa mikopo ya jumla ya Sh milioni 330.1 kwa vikundi 28 katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2026 kupitia dirisha la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 24, 2026 mjini Magu na Mkuu wa wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari 1 hadi Juni 30, 2026 kwa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Magu.

Hatua hiyo ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa ilani kwa kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwa wananchi zinatekelezwa kwa vitendo na kuchochea maendeleo pamoja na ustawi wa wananchi katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Pamoja na mambo mengine mkuu huyo wa wilaya amesema kwa upande wa kilimo, elimu ya ugani imetolewa kwa wakulima ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026 jumla ya wakulima 1,919 wamefikiwa.

“Kwa upande wa elimu ya awali na msingi, udahili wa wanafunzi wa darasa la awali umeongezeka ambapo jumla ya wanafunzi 14,952 (7,401 (wa kiume) na 7,476 (wa kike) sawa na asilimia 93.63 walidahiliwa. Upatikanaji wa vifaa vya kufundishia umeongezeka hadi asilimia 85 kwa kipindi cha Januari-Juni 2026, idadi ya shule za elimu ya awali na msingi imeongezeka kutoka 111 hadi kufikia 113 mwezi juni 2026,” amesema.

Aidha, kwa upande wa elimu ya sekondari, amesema idadi ya shule za sekondari zimeongezeka kutoka 42 na kufikia 46 Juni 2026 huku idadi ya madarasa ya sekondari ikiongezeka kutoka 765 na kufikia 793 Juni 2026.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Magu, Enos Kalambo, Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Magu imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani hapa kwa fedha kutoka Serikali Kuu. Miradi hiyo inahusu sekta za afya, maji, elimu, umeme na barabara.

Miradi hiyo imeelezwa kuwa imeleta chachu katika kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi, huku baadhi ikiwa imekamilika na mingine ikiendelea kutekelezwa.

Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Magu, Kalambo amewapongeza wasimamizi wa miradi hiyo, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jabilate Lawuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Mohamed Ramadhani pamoja na timu ya wataalam kwa usimamizi na utekelezaji wenye ufanisi.

Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Magu imewataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha miradi yote ambayo fedha zake tayari zimetolewa inakamilishwa kwa wakati, kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha, ili wananchi waanze kunufaika na huduma zilizokusudiwa.