You are currently viewing Mahakama yatupa rufani dhidi ya IPTL

Mahakama yatupa rufani dhidi ya IPTL

Mahakama ya Rufani nchini, imetupilia mbali rufani iliyowasilishwa na Benki za Standard Chartered Hong Kong (SCBH) na Standard Chartered Bank Malaysia Berhad, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

Pingamizi hilo lilihusu mahakama kukataa kusajili hukumu ya kigeni iliyoamuru IPTL na wenzake kulipa Dola za Marekani milioni168.8 sawa na zaidi ya Sh 412.87 bilioni za Kitanzania.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita chini ya jopo la majaji watatu, Jaji Mary Levira, Jaji Leila Mgonya na Jaji Gerson Mdemu ambao baada ya kusikiliza pingamizi lililowasilishwa na wajibu maombi waliona halina mashiko.

Kwenye shauri hiyo, mrufani Benki za Standard Chartered Hong Kong (SCBH) na Standard Chartered Bank Malaysia Berhad dhidi ya wajibu maombi kampuni ya Independent Power Solution Limited na VIP Engineering na Marketing Limited.

Warufani hao waliwasilisha hoja ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara wa kukataa usajili wa hukumu ya kigeni ya Mahakama Kuu ya Biashara ya Uingereza, Mahakama ya Queen’s Bench Division – Commercial Court) iliyoamuru IPTL kuilipa Benki za Standard Chartered Hong Kong Dola za Marekani Dola milioni 168.8.

Inaelezwa kuwa Februari 14,2025 mjibu maombi namba moja na mbili waliwasilisha pingamizi la awali wakiwa na sababu za kupinga rufani na kuomba itupiliwe mbali.

Hoja ya kwanza ya pingamizi wajibu maombi walidai rufani iliyowasilishwa na warufani haina uhalali wa kisheria kwa kuwa ni kinyume na Kanuni ya 97(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa, ambapo wajibu maombi namba 1 na 2 hawakupewa hati ya rufani.

Wakati hoja ya pili walidai rufani iliwasilishwa kimakosa kwa kuwa inakiuka masharti ya Kanuni ya 90(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa kwani barua ya kuomba nakala ya uamuzi na amri iliyoandikwa iliwasilishwa nje ya muda uliowekwa.

Pia, wajibu maombi walidai kuwa katika hoja ya mwisho kwamba rufani haiwezi kuendelea kisheria kuwa kuwa imepitwa na wakati kwa sababu sehemu ya madai ya mrufani tayari imeshalipwa kwa mujibu wa dhamana ya mamlaka ya Serikali.

Ilidaiwa kuwa mahakama hiyo ina makosa kimamlaka ya kuendelea kwa kuwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, ilishatoa amri katika madai hayo, kwenye shauri namba 90 la mwaka 2018 wakati rufani ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Jopo la majaji katika uamuzi wake baada ya kusikiliza pingamizi na majibu ya warufani wakipinga hoja za pingamizi ilikubaliana na pingamizi la kwanza.

“Kwa kuongozwa na kanuni ya sheria iliyoanishwa hapo juu na baada ya kukubali pingamizi la awali la kwanza, tunaona pia kwamba rufaa hii si halali kisheria hivyo basi, tunalazimika kuifuta pamoja na gharama zake,”

Kwenye shauri hiyo, warufani waliwakilishwa na mawakili Gaspar Nyika, Deogratius Tesha na Edna Mwankenja huku wajibu maombi wa kwanza na pili wakiwakilishwa na wakili Mussa Mhagama na mjibu maombi wa tatu aliwakilishwa na Dosca Mutabuzi, Michael Ngalo, Prescius Didace na Deogratius Mwarabu.

Leave a Reply