Mamlaka ya kitaifa ya kusimamia safari za ndege nchini Marekani jana Jumanne imetangaza kuwa itapiga marufuku safari za ndege za Marekani kuelekea Haiti kwa siku 30 baada ya ndege ya shirika la Spirit Airlines kushambuliwa kwa risasi na magenge yenye silaha.
Umoja wa Mataifa pia umesema kuwa utasitisha safari za ndege nchini humo, hali ambayo huenda ikaathiri upelekaji wa misaada pamoja na wafanyakazi wa misaada.
Ndege iliyoshambuliwa iligongwa kwa risasi wakati ilipokuwa karibu kutua Jumatatu kwenye mji mkuu wa Haiti wa Port au-Prince, huku mmoja wa wafanyakazi wake akijeruhiwa.
Ghasia mpya zimezuka nchini humo baada ya kuapishwa kwa waziri mkuu mpya, kufuatia mchakato ulioghubikwa na siasa kali. Maisha kwenye sehemu nyingi za mji huo mkuu yalivurugika kufuatia ghasia hizo na mambo yakachukua mrengo mwingine baada ya ndege hiyo kushambuliwa, huku uwanja wa ndege ukilazimika kusitisha shughuli zake.
Picha na video zilizoonyeshwa shirika la habari la AP, zilionyesha mashimo ya risasi ndani ya ndege hiyo. Mashirika mengi ya ndege yamesitisha safari zao hadi Alhamisi, ingawa haijulikani ni kwa muda gani uwanja huo utabaki kufungwa.
Waziri mkuu wa zamani Gary Conille wala waziri mpya Alix Didier Fils-Aime hawajasema lolote kuhusu tukio hilo kufikia sasa.