Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni, amesema biashara ya hewa ukaa inatarajiwa kufungua fursa za ajira na kuongeza kipato kwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini, kupitia shughuli mbalimbali za upandaji na utunzaji wa miti.
Amesema mnyororo mzima wa biashara hiyo, kuanzia utayarishaji wa miche, upandaji, utunzaji wa miti hadi kuiingiza katika soko la hewa ukaa, una fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kuwapatia wananchi ajira na kipato.
Masauni amesema amekuwa akilielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Kituo cha Taifa cha Kusimamia Biashara ya Kaboni kuhakikisha wananchi wanaelimishwa kuhusu fursa zilizopo na namna wanavyoweza kuzitumia kujinufaisha kiuchumi.
Amesisitiza kuwa biashara ya hewa ukaa ina manufaa mawili makubwa, ikiwemo kuchangia uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji na utunzaji wa miti, pamoja na kuongeza kipato na ajira kwa wananchi wanaoshiriki katika shughuli hizo.
Aidha, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada za kuimarisha biashara hiyo nchini, ikiwemo kuanzisha kituo maalumu cha kusimamia biashara ya kaboni na kufanya maboresho ya sera na sheria ili kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa shughuli hizo.#TanzaniaCOP31
