Wakazi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wanatarajiwa kukabiliwa na upungufu wa huduma ya maji kwa siku nne kuanzia Novemba 3 hadi 6, 2026, wakati Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ikifanya matengenezo ya bomba kuu lenye kipenyo cha inchi 72 linalopokea maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi Everlasting Lyaro imesema matengenezo hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha miundombinu yake ya majisafi kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Kutokana na kazi hiyo, uzalishaji wa maji katika mtambo huo utapungua kwa asilimia 60 kwa kipindi cha saa 96, hali inayotarajiwa kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wakazi wanaohudumiwa kupitia chanzo hicho.
Maeneo yatakayoathirika ni pamoja na Zinga, Kiromo, Dunda, Kisutu, Magomeni, Nianjema, Fukayosi, Makurunge, Kerege, Mapinga, Mbweni, Mabopwepande, Bunju, Kunduchi, Kawe, Mbezi Juu, Goba, Wazo, Makongo, Kijitonyama, Kinondoni, Makumbusho, Msasani, Mzimuni, Tandale, Ndugumbi, Kigogo, Magomeni, Kariakoo, Mchikichini, Upanga Magharibi, Gerezani, Upanga Mashariki, Kisutu, Mchafukoge, Jangwani, Kivukoni, Ilala, Mnyamani, Liwiti, Kilungule, Kilakala, Mianzini, Keko, Kurasini, Miburani na Chang’ombe.
DAWASA imewaomba wateja na wananchi katika maeneo hayo kuvumilia usumbufu utakaoweza kujitokeza wakati wa matengenezo hayo, huku ikiwahimiza kupanga matumizi ya maji na kuhifadhi kiasi cha kutosha kwa matumizi muhimu kabla ya kazi kuanza.
DAWASA imewaomba wakazi hao kuhifadhi Maji ya kutosha wakati kazi ya matengenezo itakapofanyika.
