Na Mwandishi Wetu, Kigoma
IMEELEZWA kuwa matumizi ya nishati ya umeme katika mkoa wa Kigoma yameongezeka kutoka Megawati 17 hadi kufikia Megawati 24 baada mkoa huo kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa ya umeme Disemba 2024.
Hayo yamebainishwa jana Jumanne na Mkuu wa mkoa huo, Simon Siro katika ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange mkoani humo.

“Ongezeko hili linaonesha wazi kwamba kulikuwepo na uhitaji mkubwa wa umeme katika Mkoa wa Kigoma. Kuunganishwa kwa Mkoa huu na Gridi ya Taifa kumeleta mabadiliko chanya”, alieleza Twange.
Aidha, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa TANESCO iko tayari kushughulikia changamoto zozote za umeme zitakazojitokeza kwa wakati, ili kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana bila usumbufu.
“Niwahakikishie wakazi wa Kigoma kuwa TANESCO itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kilimo, biashara na matumizi ya majumbani,” alisema Bw. Twange.
Pia, katika kuunga mkono jitihada ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Bw. Twange alikabidhi majiko ya umeme kwa familia ya Mkuu wa mkoa huo pamoja na familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye na kuwaomba watumie vifaa hivyo kama mfano kwa jamii.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Malagarasi (MW 49.5) pamoja na Kituo cha Kupooza Umeme cha Kidahwe. Alieleza kuwa TANESCO inaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
“Ninamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu wa Malagarasi. Hadi sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 10 na kazi inaendelea vizuri,” aliongeza Bw. Twange.
Ziara ya Mkurugenzi Mtendaji inalenga kufuatilia na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya TANESCO katika mikoa ya Kanda ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Kigoma.