Mwanzilishi wa kampuni ya kutengeneza pikipiki ya ZXMOTO nchini China, Zhang Xue, ameweka historia baada ya kuendesha pikipiki maalumu iliyofanyiwa marekebisho umbali wa kilomita 40.74 juu ya maji, na kuweka rekodi mpya ya dunia inayotambuliwa na Kitabu cha Rekodi za Dunia cha Guinness.
Zhang aliweka rekodi hiyo jana Jumapili katika Wilaya ya Mayang Miao, Mkoa wa Hunan, katikati mwa China, ambako alitumia pikipiki aina ya ZXMOTO MX450 iliyofanyiwa marekebisho maalumu ili iweze kutembea juu ya maji.
Katika jaribio hilo, Zhang aliendesha pikipiki hiyo kwa kupita na kurudi katika mto, akifanikiwa kutimiza umbali wa kilomita 40.74 na kuweka rekodi ya umbali mrefu zaidi kuwahi kufikiwa na pikipiki iliyofanyiwa marekebisho maalumu wakati wa kutembea juu ya maji.
Akizungumzia mafanikio hayo, Zhang alisema alikuwa na imani kubwa kuwa angeweza kutimiza azma yake, licha ya changamoto zilizokuwa mbele yake.

“Nina imani kubwa kuwa ninaweza kufanikisha jambo hili. Hata nikishindwa, sitaacha kulifuatilia. Ninafurahia sana mchakato mzima wa kulitimiza,” alisema.
Mafanikio hayo ni matokeo ya safari ya muda mrefu iliyoanza mwaka 2009, wakati Zhang alipoanza majaribio ya kuendesha pikipiki juu ya maji kwa kutumia teknolojia na vifaa vya kawaida alivyokuwa amevifanyia marekebisho.
Katika jaribio lake la kwanza, aliangukia majini mara nne na kufanikiwa kusafiri umbali usiozidi mita 20, hali ambayo haikumvunja moyo bali ilimpa msukumo wa kuendelea kuboresha ubunifu wake.
Kwa ajili ya jaribio la kihistoria la Jumapili, pikipiki aina ya MX450 iliwekewa vifaa maalumu vinavyoiwezesha kuelea na kusafiri juu ya maji, ikiwemo skii maalumu za kutembea majini, tanki kubwa zaidi la mafuta pamoja na mifumo ya ziada ya kuzuia maji yasiingie kwenye sehemu muhimu za injini.
Mfumo wa uendeshaji wake unaiwezesha pikipiki hiyo kupata kasi ikiwa nchi kavu kabla ya kuingia majini na kuendelea kusafiri juu ya uso wa maji. Kifaa maalumu kilichowekwa mbele husaidia kuelekeza pikipiki, huku tairi la nyuma likisukuma maji kuelekea nyuma na kuiwezesha kusonga mbele.
Zhang alisema kufanya jaribio hilo katika eneo alikozaliwa kuliongeza thamani na maana ya mafanikio hayo, akieleza kuwa alitaka pia kuitangaza wilaya yake kwa jamii ya kimataifa.
“Roho ya uvumilivu na kutokukata tamaa inatokana na ardhi hii. Kwa kuleta changamoto hii katika mji wangu wa nyumbani, nilitaka pia kutimiza ndoto yangu hapa na kuifanya dunia iifahamu Mayang,” alisema.
Mafanikio ya Zhang yanaonesha namna ambavyo uvumilivu, ubunifu na dhamira ya kutokata tamaa vinavyoweza kumwezesha mtu kubadili changamoto za muda mrefu kuwa mafanikio yanayovutia dunia.
