Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kumalizika kwa mkataba wa ununuzi wa umeme kutoka Kampuni ya uzalishaji umeme kwa njia ya Gesi asilia ya Songas.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Kurugenzi ya Mawasiliano TANESCO imeena mkataba huo umedumu kwa muda wa miaka 20 na umefikia ukomo wake jana tarehe 31 Oktoba 2024.
Pamoja na kufika ukomo wa mkataba huu Shirika linapenda kuwahakikisha wateja wake kuwa hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni nzuri kwa kuzingatia vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme ambapo kwa sasa uwezo wa uzalishaji umeme kwa kutumia mitambo ya Gesi asilia na mitambo inayotumia maji ni mkubwa kuliko mahilaji ya umeme hapa nchini.
Imesema hali hiyo imechangiwa na maendeleo mazuri ya Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo mpaka sasa jumla ya megawati 940 zimeungwa kwenye Gridi ya Taifa.
Maamuzi ya Serikali kutokuendelea na mkataba huu ni kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya nchi.
“Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO itaendelea kusimamia sekta ndogo ya umeme ili kuhakikisha kunakuwa na huduma bora, endelevu na ya uhakika ya umeme,” imesema taarifa hiyo.