Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma imetupilia mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanachama wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina pamoja na ACT- Wazalendo kupinga kuondolewa kwenye orodha ya wagombea Urais wa Tanzania.
Mahakama imeeleza kuwa haina mamlaka ya kuingilia uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) unaotekelezwa kwa mujibu wa Katiba na sheria.
Shauri hilo limesikilizwa mbele ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Frederick Mayanda, huku upande wa waleta maombi ukiongozwa na Wakili John Seka na timu yake ya mawakili. Wadaiwa katika shauri hilo walikuwa ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ofisi ya mwanasheria mkuu wa chama hicho, imeeleza kuwa ACT Wazalendo kitachukua hatua za kisheria ikiwemo kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, kuwafikia na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuendelea kupigania mabadiliko ya kisheria na kikatika kwenye uchaguzi.
Kwa uamuzi huo, Mpina hataweza kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, ambao kwa sasa vyama vya siasa vinavyoshiriki vinaendelea na kampeni.