LICHA ya Timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Timu ya taifa ya Congo (DRC), Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amesema Taifa Stars bado ina nafasi kuwania kufuzu michuano ya AFCON 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jana usiku, Waziri huyo amesema Tanzania bado ina nafasi kwa michezo iliyobaki kama itashinda hivyo wasikatishwe tamaa na matokeo hayo.
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilikubali kichapo hicho dakika za mwisho kutoka kwa Timu ya Taifa ya Congo licha ya kucheza nyumbani katika dimba la Benjamini Mkapa na kushuhudiwa na Waziri mkuu, Kassim Majaliwa.
Kwa matokeo hayo, sasa Taifa Stars inashika nafasi ya tatu baada ya Timu ya Taifa ya Guinea kuitandika Ethiopia bao 3 bila mtungi na kufikisha pointi sita huku Tanzania ikibakiwa na alama nne. Congo inaongoza kundi kwa alama 12 na kujihakikishia kufuzu hukiu Ethiopia wakipoteza matumaini kwa kubaki na alama 1.