Na Mwandishi Wetu, Kigali – Rwanza
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia katika ushirikiano wa kimkakati wa kifedha wenye thamani ya dola za Marekani milioni 15, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 40, na taasisi ya British International Investment (BII) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa biashara ndogo, za kati na za kati (MSMEs) nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yaliyotangazwa pembezoni mwa Mkutano wa Africa CEO Forum 2026 unaofanyika Kigali, Rwanda, yatahusisha utoaji wa ufadhili wa muda mrefu kwa kipindi cha miaka mitano ili kusaidia ukuaji wa biashara, kuimarisha uthabiti wa kiuchumi na kuongeza ushindani wa biashara za Kitanzania katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ilishuhudiwa na Waziri wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, aliyeiwakilisha Serikali ya Tanzania ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa za Benki ya NBC. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi, pamoja na Mkurugenzi Mkuu na Mkuu wa Kanda ya Afrika wa BII, Chris Chijiutomi.
Kupitia mpango huo, wafanyabiashara wadogo na wa kati watanufaika na upatikanaji wa mtaji wa kuendesha biashara, huduma za kifedha kwa biashara za ndani na za kimataifa pamoja na suluhisho bunifu za kifedha zitakazowezesha biashara hizo kukua na kushindana katika soko la kikanda. Ufadhili huo pia utaongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kiuchumi kwa kusaidia urasimishaji wa biashara, matumizi ya teknolojia za kidijitali na ushiriki katika biashara za kikanda chini ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Sabi alisema ushirikiano huo unaashiria kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kimataifa katika sekta binafsi ya Tanzania pamoja na mchango wa taasisi za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.
“Biashara ndogo na za kati zinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika ajira, uzalishaji na maendeleo ya ujasiriamali. Ushirikiano huu ni zaidi ya ufadhili wa kifedha; ni uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kuwezesha biashara za Kitanzania kupata mitaji na suluhisho stahiki za kifedha ili ziweze kupanuka na kushindana katika soko la kikanda,” alisema.
Aliongeza kuwa NBC itaendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya taifa kwa kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wafanyabiashara nchini.
Kwa upande wake, Waziri Kairuki alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji, ubunifu na ushindani wa biashara za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
“Ushirikiano huu baina ya Benki ya NBC na BII una mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, kuimarisha ujasiriamali na kukuza ushiriki wa biashara za Kitanzania katika uchumi wa kikanda na wa kimataifa,” alisema.
Naye Chris Chijiutomi alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya BII katika kusaidia biashara ambazo bado zinakabiliwa na changamoto ya kupata huduma za kifedha, akibainisha kuwa mpango huo utasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi, ubunifu na ajira nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu za sekta hiyo, biashara ndogo na za kati zinachangia zaidi ya asilimia 90 ya biashara zote nchini Tanzania na kati ya asilimia 27 hadi 35 ya Pato la Taifa (GDP), huku zikitoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania.
Mkutano wa Africa CEO Forum 2026 umewakutanisha watunga sera, wawekezaji, taasisi za fedha za maendeleo pamoja na viongozi wa biashara kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kujadili mageuzi ya uchumi wa Afrika, fursa za uwekezaji na ukuaji wa sekta binafsi.
