You are currently viewing NFRA yajiandaa kukabiliana na upungufu wa sukari nchini 

NFRA yajiandaa kukabiliana na upungufu wa sukari nchini 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) umesema  umejipanga vizuri  kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini endapo  kutajitokeza upungufu  wa bidhaa  hiyo kwani serikali imeshatoa  kibali  kwa wakala kuagiza na kusambaza sukari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Andrew Komba alisema NFRA imepewa  jukumu la ununuzi wa sukari nje  kwa ajili ya kutosheleza soko la ndani pale uhaba utakapojitokeza kwa lengo la kuwa na akiba ya kutosha kwa kipindi cha miezi miwili kama sheria ya sukari inavyosema.

Sheria ya sukari inasema kwamba, “endapo NFRA itagundua kuna uhaba wa sukari itatoa sukari yake iliyoihifadhi na kuiingiza sokoni,”

 “Lakini pia endapo mojawapo ya kiwanda au viwanda vyote vikashindwa kuzalisha, basi NFRA itatoa sukari yake iliyoiagiza na kuiingiza sokoni” alisisitiza Dkt Komba.

Dk. Komba alibainisha kwamba Bunge lilipitisha sheria hiyo na kuipa nguvu taasisi hiyo kuwa na sukari ya kutosha muda wote na siyo kusubiri mpaka pale kunapokuwa na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.

“Malengo ya Serikali ni kuona Watanzaia wanapata mahitaji muhimu na kuhakikisha uwepo kwa akiba ya chakula cha kutosha ikiwemo sukari kwa usalama wa nchi. 

“Na ndiyo maana baada ya kujengewa uwezo wa kutosha na Serikali, NFRA imeweza kuwa na akiba ya kutosha ya chakula ikiwemo sukari katika kukabiliana na upungufu wowote unaoweza kujitokeza,” amesema.

Dk. Komba alisema  kwa upande wa nafaka, wakala umeweza kuhifadhi akiba ya kutosha ya chakula  ziada kuuza nje ya nchi.

 “Lakini pia kwa upande wa sukari, tunahakikisha kuwa ipo ya kutosha ili kukabiliana na upungufu hasa pale viwanda vinaposhindwa kuzalisha au kuagiza  kutoka nje ili kuhakikisha nchi inakuwa na bidhaa hiyo muhimu muda wote ili kukabiliana na upungufu unaoweza kujitokeza,” amesema Dk. Komba.

Amesema kuwa Serikali imeipa taasisi yake mamlaka ya ununuzi na kuhifadhi sukari kutokana na changamoto ya uhaba wa bidhaa hiyo kujitokeza mara kwa mara miaka iliyopita na kuleta usumbufu kwa wananchi.

“Tumelipokea jukumu hili kwa mikono miwili na utekelezaji wake unakwenda vizuri,” amesema Dk. Komba.

Mwaka jana, wakati Rais Samia  alipokuwa ziarani mkoani Morogoro, alifungua kiwanda cha sukari cha Mkulanzi ambacho kinamilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, ambapo alisema kuwa lengo la uwepo wa kiwanda hicho  ni kuongeza kiasi cha uzalishaji sukari hapa nchini.

Wakati wa ziara hiyo, Rais  Samia alisema kuwa kati ya mwezi Machi mpaka Mei (mwaka Jana), kulikuwa na upungufu wa sukari, hivyo serikali ikaagiza sukari nje ya kutosha na kupelekea bei yake kushuka ili kuwasadiai wananchi kuipata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

Aidha, Dk. Komba alisema  serikali kupitia Waziri wa Kilimo Bw. Hussein Bashe ilisema kuwa katika kukabiliana na upungufu wa sukari uliokuwa unajitokeza, serikali  ipo tayari kufanya kazi na taasisi binafsi kwa ajili ya kuhakikisha sukari inapatikana  kw uhakika nchini na kuwataka wafanyabiashara wawe waaminifu na wasipandishe bei ya sukari.

Viwanda vinavyozalisha sukari hapa nchini ni pamoja na kiwanda cha Kilombero, Mtibwa, Bagamoyo, TPC Limited na  kiwanda cha Serikali cha Mkulazi.

Leave a Reply