Na Mwandishi Wetu, Marekani.
Benki ya NMB imesaini makubaliano na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) na Mastercard kuzindua Mradi wa Ushauri wa “Banking on Women Advisory Project,” ambao unalenga kuboresha masuluhisho ya kifedha kwa wanawake nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yamesainiwa jana Alhamisi, tarehe 24 Oktoba 2024, katika Mkutano wa Mwaka wa Shirika la IFC na Benki ya Dunia unaofanyika Washington, DC, Marekani. Ujumbe wa benki ya NMB katika hafla hii ya utiaji saini uliongozwa na Afisa Mkuu wa Fedha, Juma Kimori aliembatana na Mhazini, Aziz Chacha na Meneja Mwandamizi wa Bidhaa, Beatrice Mwambije.
Mradi huu wa miaka minne unalenga kuja na masuluhisho ya kifedha yanayokidhi mahitaji ya wanawake au biashara zinazomilikiwa na wanawake nchini ikiwemo huduma mahsusi, mikopo nafuu na elimu ya kifedha.
Kupitia makubaliano haya, wafanyakazi wa Benki ya NMB pia watapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuendelea kubaini fursa za kubuni masuluhisho zaidi yanayozingatia mahitaji ya kifedha na yasiyo ya kifedha ya wanawake nchini ili kuimarisha mchango wa kundi hili katika ustawi wa jamii na uchumi wa Taifa.
Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika mkakati wa benki ya NMB katika ujumuishwaji wa kifedha wa Watanzania, kupitia kampeni yao ya “Sisi ni Huduma #tumekupata”.