Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya NMB na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wamesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha benki hiyo kusaidia gharama za matibabu ya watoto wanaotibiwa katika taasisi hiyo kwa kiasi cha Sh. Bilioni 1 kwa miaka minne, sawa na Sh. Milioni 250 kwa mwaka.
Makubaliano hayo yamesainiwa jana Alhamisi Oktoba 31, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, mbele ya wanasheria wa taasisi hizo.
Akizungumza wakati wa utilianaji Saini huo, Bi. Zaipuna alisema Sekta ya Afya ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa taasisi yake, ambayo inatambua na kuthamini juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo inachangia asilimia 70 ya matibabu ya watoto hao.
Alibainisha kuwa, kwa mujibu wa makubaliano waliyosaini, NMB inaenda kusaidia asilimia 30 ya gharama za matibabu, ambayo ni takribani Sh. Mil. 4 kwa mtoto mmoja, ambayo bado ni kubwa kwa wazazi na walezi wengi nchini kumudu kulipa na kuwezesha tiba kwa watoto wao.
“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, zaidi ya watoto 13,800 huzaliwa na changamoto za moyo kwa mwaka hapa Tanzania, wengi miongoni mwa wazazi wa watoto hao wanashindwa kumudu gharama za matibabu, na hivyo watoto wengi huchelewa kupata matibabu stahiki na hivyo afya zao kuwa mashakani.
“Sasa kwa makubaliano haya, NMB itachangia kiasi cha Sh. Bilioni Moja kwa kipindi cha miaka minne, ambapo kila mwaka tutachangia Sh. Mil. 250 kuanzia mwaka huu na tuna imani mchango huu utakuwa msaada mkubwa hasa kwa wazazi wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu ya watoto hawa,” alisema.
Bi. Zaipuna alifafanua kwamba pamoja na mchango huo wa fedha taslim, NMB pia itashirikiana na JKCI, kuwezesha wataalamu wa Magonjwa ya Moyo wa taasisi hiyo kutoa elimu ya Magonjwa ya Moyo kwa wafanyakazi wa benki hiyo, wateja, pamoja na wadau wengine ili kusaidia kuongeza ufahamu wa Afya ya Moyo kwa Watanzania.
“NMB pia tutakuwa na wajibu wa kushiriki katika shughuli nyingine mbalimbali za kusaidia upatikanaji wa fedha zaidi zitakazowezesha matibabu ya watoto wanaotibiwa hapa kwa kushirikisha wadau wengine. Kwa hiyo huu ni mwanzo tu, kwa mashirikiano haya ya NMB na JKCI,” aliongeza.
Aidha, aliipongeza JKCI na HTAF kwa kazi kubwa wanayofanya kwa watoto wa Kitanzania na kwamba NMB inajivunia kuwa Mshirika Mkuu wa taasisi hizo mbili katika kutatua changamoto ya afya ya moyo na kurejesha tabasamu za watoto wenye maradhi hayo, huku akiwataka wadau wa afya nchini kuunga mkono jambo hilo.
Makubaliano haya ni muendelezo NMB na Taasisi za Serikali, ambapo mwaka jana NMB ilifanya ukarabati mkubwa Wodi ya Wazazi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), uliojumuisha pia uwekaji wa vifaa vipya na vya kisasa kwenye wodi hiyo iliyoko Jengo ambalo sasa linaitwa Jengo la Uzazi la NMB.
Kabla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Dk. Kisenge aliishukuru NMB kwa kukubali kuingia makubaliano hayo, aliyoyataja kama yanayoenda kuunga mkono juhudi za Rais Dk, Samia Suluhu Hassan, aliyempongeza kwa kufanya mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya nchini hususani JKCI.
“Dk. Samia amefanya makubwa sana katika Sekta ya Afya na JKCI ni miongoni mwa mnufaika wa juhudi hizo, mapinduzi aliyoleta yanaifanya JKCI kuwa taasisi kubwa na ya kwanza Afrika linapokuja suala la tiba za maradhi ya moyo, oparesheni salama na uokozi wa vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo, ambavyo viko chini ya asilimia 5.
Alibainisha ya kwamba Historia ya JKCI haiwezi kuelezewa popote bila kuitaja NMB, ambayo imefanya makubwa hapo tangu 2015, ambako imesaidia sio tu wagonjwa wanaotibiwa hapo, bali hata wafanyakazi wa taasisi kwa kuwapa huduma bora na rafiki, ikiwemo mikopo nafuu inayowaongezea ufanisi kazini.
“Kuthibitisha kuwa huu ni muendelezo, mwaka 2017 NMB ilijenga eneo la mapunziko ya wagonmjwa wa nje chini ya uongozi wa Profesa Mohamed Janabi, lakini mwaka 2022 wafanyakazi wa NMB walichanga sehemu ya mishahara yao kusaidia gharama za matibabu ya watto waliofanyiwa opearesheni hapa.
“Mwaka 2023, Bi. Zaipuna alikuja hapa kushiriki Siku ya Wanawake Duniani, ambapo alitoa mchango mkubwa wa vifaa tiba, yakiwemo mashuka kwa wagonjwa, hii inaakisi ukweli kuwa NMB inajali wagonjwa, sio tu wa hapa JKCI, bali sekta nzima ya afya nchini kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR),” alisema.
Dk. Kisenge aliahidi kwamba JKCI itazingatia makubaliano yaliyosainiwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu juu ya maradhi ya moyo, na kwamba wataendelea walipoishia kwa sababu tayari taasisi yake imeshazunguka katika mikoa 17 na kuonana na kusaidia wagonjwa zaidi ya 17,000.
“Nia ya ziara zetu mikoani ni kuwafikia waliko na kuwapunguzia mzigo wa kutufuata, tunaahidi ushirikiano mwema na NMB, ambayo wateja wenye kadi za ‘premium’ za benki hii watatibiwa JKCI. Tunashukuru kwa namna NMB inavyojitoa kwa Watanzania, pia kwa jinsi inavyosaidia juhudi za Rais Samia.