You are currently viewing NMB, Wakandi waungana kuviwezesha vyama vya akiba na mikopo

NMB, Wakandi waungana kuviwezesha vyama vya akiba na mikopo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KWA kutambua umuhimu na mchango wa Vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos) kwa maendeleo ya vikundi na mwanachama mmoja mmoja, Benki ya NMB imeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni inayotoa huduma za kifedha kigitali ya Wakandi Tanzania Limited, unaolenga kuleta suluhishi maalum za kibenki kwa vyama hivyo.

Makubaliano hayo yamezinduliwa jijini Dar es Salaam leo Jumatano Oktoba 9, ambapo kupitia ushirikiano huo, wanachama wa Saccos watachangia, kuweka akiba na kulipa mikopo yao kupitia njia NMB Mkononi, NMB Wakala na Matawi 231 ya benki NMB yaliyopo kote nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Mabadiliko ya Kidigitali wa Benki ya NMB, Kwame Makundi, alisema kupitia masuluhisho maalum yaliyobuniwa, Saccos zitanufaika katika maeneo mengi, ikiwemo kupata taarifa za miamala ya akaunti zao kupitia mfumo maalum.

“Faida nyingine ni pamoja na Saccos kudhibiti mapato yao, kwani malipo yatafanywa kwa kutumia namba za malipo (control number), lakini pia zitaboresha ufanisi kwa kupunguza kazi na gharama za uendeshaji katika Saccos zilizo chini ya Wakandi Tanzania,” alisema

Makundi aliongeza kwa kueleza kuwa, kwa mujibu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Ripoti ya Mwaka ya Utendaji wa Saccos na Usimamizi kwa Mwaka 2022, inaonesha kuwa kuna Vyama vya Akiba na Mikopo vilivyopata leseni kufikia mwaka huo vilikuwa 801.

“Idadi ya wanachama iliongezeka kutoka milioni 1.3 mwaka 2021 hadi wanachama milioni 1.8 mwaka 2022, sawa na ukuaji wa asilimia 38, hii inamaanisha kwamba hadi kufikia mwaka huu wa 2022, idadi hiyo imeongezeka sana na hii inaonesha jinsi Saccos zilivyo muhimu katika jamii yetu.

“Kwa mantiki hiyo suluhishi hizi ni muhimu kwa ustawi wa vikundi hivi, hasa ukizingatia kuwa Saccos zimekuwa na mchango mkubwa kwa watu binafsi, familia, wafanyabiashara, wajasiriamali, wafanyakazi kupanga mikakati ya maendeleo kupitia akiba na mikopo,” alisisitiza.

Makundi alibainisha kuwa, masuluhisho yatokanayo na ushirikiano baina ya MB na Wakandi Tanzania Limited, hayatoishia tu kubadili namna ya usimamizi wa fedha za vikundi, bali pia wanachama watapata kujengewa uelewa juu ya Saccos na Elimu ya Fedha.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakandi Tanzania Limited, Espen Kvelland, aliishukuru NMB kwa kukubali kusaini na kuzindua ushirikiano baina yao, alioutaja unasadifu falsafa isemayo; ‘Ukitaka uwenda haraka tembea peke yako, ila ukitaka kwenda mbali zaidi ambatana na wenzako.’

“Tunaamini katika upana wa mtandao wa matawi, mawakala, na ubora wa huduma za NMB, taasisi ambayo imefanya uwekezaji mkubwa sana katika mifumo ya kidigitali, hivyo mani yetu ni kuwa ushirikiano baina yetu utasaidia kuharakisha hatua za kimaendeleo kwa vyama vyetu na wanamachama wake,” alisema.

Alibainisha ya kuwa, ushirikiano huo baina ya taasisi yake na NMB unaenda kuweka uwazi katika michakato mizima ya uwekaji akiba, ukopaji na urejeshaji wa mikopo hiyo, kupitia mifumo ya kidigitali na kumaliza kabisa changamoto za awali za vikundi kukopeshana kwa njia zisizo salama kwa ukuaji wa vyama.

Kwa upande wake, Meneja wa DART Sacco, Jofrey Kengese, akizungumza kwa niaba ya vyama vingine vilivyo chini ya Wakandi Tanzania Limited, mashirikiano baina yao na Wakandi yaliwapunguzia upotevu wa kumbukumbu muhimu na kwamba NMB inaenda kuwaondoa kabisa katika changamoto hizo na nyinginezo.

“Tunaamini ushirikiano huu unaenda kufupisha kipindi cha kusubiria mchakato, kuondoa uwekezano wa kukosea ujazaji wa taarifa za akaunti ya benki na naamini mashirikiano haya yatawezesha mpango mkakati uliopo unaolenga kufanikisha uombaji wa mikopo na upataji ndani ya dakika tano tu,” alisema Jofrey. 

Saccos wanachama wa Wakandi ni DART Saccos Ltd, DSM Corridor Saccos Ltd, Wakandi Saccos, MKUTA Saccos Ltd, Tujiajiri Saccos Ltd, Long Farmers Saccos Ltd, Kumekucha Saccos Ltd, Endeleza Credit Facility Ltd, MUHAS Alumni Saccos Ltd, TDFT Microfinance Ltd na nyinginezo.

Leave a Reply