Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya NMB imetangaza gawio la kihistoria kwa wanahisa la Sh. bilioni 214.43 na kufikia jumla ya gawio la Mwaka la Sh. bilioni 214.43 kwa wanahisa wake kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2024.
Pendekezo na uamuzi huo umepitishwa leo Alhamisi katika Mkutano Mkuu wa 25 wa wanahisa uliofanyika kidijitali jijini Dar es Salaam huku malipo ya gawio hilo yakitarajiwa kufanyika tarehe 19 Juni 2025 au muda mfupi baada ya hapo, ukiwa ni mwaka mwingine wa kuwahakikishia wanahisa thamani endelevu.

Katika taarifa ya benki hiyo, imeonesha kuwa malipo ya gawio la Sh. bilioni 214.43 ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na malipo ya gawio lililolipwa mwaka 2023 la Sh. bilioni 180.59
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB, Davida amesema mwaka 2024, benki hiyo iliendelea na mwendo mzuri wa utendaji ambapo benki ilipata faida baada ya kodi ya Sh. bilioni 643 likiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Amesema utendaji mzuri wa benki uliimarisha nafasi yake ya kuendelea kuwa kiongozi na kama mmoja wa benki zinazofanya vizuri zaidi Afrika Mashariki na kiongozi wa kweli wa huduma za kifedha.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa mizania ya Benki iliendelea kuimarika kutokana na kuwa imara kimtaji. Mikopo iliongezeka kwa asilimia 10 na kufikia Sh. trilioni 8.5 kutokana na ukuaji wa ukopeshaji katika maeneo nyeti ikiwemo kilimo, sekta ya ujariamali, wateja binafsi, biashara kubwa na serikali.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth amesema amana za wateja zilifikia Sh. trilioni 9.6 likiwa ni ongezeko la asilimia 13 mwaka hadi mwaka kutokana na ukuaji wa amana katika maeneo yote nyeti ya biashara yetu.
Amesema kutokana na mwenendo mzuri wa mizania, jumla ya mali za Benki zilikua kwa asilimia 13 mwaka hadi mwaka na kufikia Sh. trilioni 13.7. Benki iliendelea kuwa imara kimtaji ikiwa ndani ya ukomo wa kikanuni na hivyo kuwa katika nafasi ya kuwa na biashara endelevu na nafasi ya uwekezaji wenye tija siku za usoni.
Akinukuu taarifa hiyo, amesema moja ya kiashiria kikuu cha kikanuni kinaonesha maendeleo makubwa ya kiuwiano katika ufanisi na maboresho kwenye ubora wa mali na uwekezaji.
“Kufikia Desemba mwaka 2024, NMB ilipata uwiano wa gharama na matumizi wa asilimia 38 ikilinganishwa na asilimia 39 ya mwaka 2023 hii ikiwa ni chini ya ukomo wa kikanuni wa asilimia 55, na kuifanya benki hiyo kuwa ni miongoni mwa benki zenye ufanisi mkubwa nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Usimamizi wa hali ya juu wa ufadhili na uwekezaji ikiwa ni pamoja na ubora wa vyanzo vya mikopo na usimamizi imara kulipelekea uwiano wa mikopo chechefu kushuka na kufikia asilimia 2.9 kutoka asilimia 3 ya mwaka uliotangulia. Uwiano huu wa benki umeendelea kuwa ndani ya ukomo wa kikanuni wa asilimia 5 na chini ya wastani wa uwiano wa kisekta,” amesema.

Awali Nchimbi alisema; “Malipo haya ya gawio yanatoa ishara thabiti ya maendeleo na ufanisi wa utekelezaji wa mkakati wetu, misingi imara ya utawala bora, na imani kubwa waliyonayo wanahisa wetu katika mipango yetu ya siku zijazo.
“Tunaendelea kujikita kwa ari katika kufungua fursa mpya za kimkakati za ukuaji wa huduma za kifedha, kuboresha na kuimarisha huduma kwa wateja wetu, na kujenga ushirikiano wa kudumu wenye tija kwa pande zote.
“Lengo letu ni kufanikisha maono makubwa ya kuwa mshirika sahihi wa masuluhisho ya kifedha yanayotoa thamani kwa wateja, wawekezaji, na wadau wote kwa ujumla, kwa kuzingatia ufanisi, uvumbuzi, na uwajibikaji wa hali ya juu,” alisema.
Nchimbi aliongeza “Kwa miaka ijayo, kupitia utekelezaji makini wa majukumu yetu ya utawala bora na uwajibikaji, Bodi ya wakurugenzi itaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa muda mrefu wa benki na kutoa thamani endelevu kwa wanahisa wetu.”
Aidha, Bi. Zaipuna aliongeza kuwa, “Mwaka 2024 ulikuwa ni mwaka wa kipekee kwa Benki ya NMB, ulioshuhudia maendeleo makubwa dhidi ya mkakati wetu, na kuongeza thamani kwa wadau wetu wote, ufanisi wa kiutendaji na malipo ya gawio hili kubwa kama ilivyopitishwa na wanahisa kunadhibitisha dhamira yetu ya kuwa na ukuaji madhubuti wenye matokeo endelevu.

“Shukrani zangu za dhati ziende kwa Serikali yetu, wasimamizi wa sekta ya fedha, wateja, wanahisa, na wafanyakazi wetu kwa mchango wao mkubwa na imani yao kwetu.
“Kutokana na ushirikiano huo, tumeanzisha na kuendeleza taasisi kubwa na endelevu, ikionyesha sifa ya kuwa kiongozi wa huduma bora kwa wateja, uvumbuzi wa kisasa, na utendaji wenye ufanisi wa hali ya juu.
“Natoa shukrani za dhati kwa kuendelea kuwa sehemu ya safari hii, na tunatarajia kuendeleza mafanikio ya pamoja kwa kuimarisha ushirikiano wetu wa kipekee, kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu na thamani kubwa kwa wadau wote,” alisema.