You are currently viewing Polisi 3 kortini mauaji ya Albert Ojwang

Polisi 3 kortini mauaji ya Albert Ojwang

Waendesha mashtaka wa Kenya wametangaza jana Jumatatu kufungua mashtaka dhidi ya watu sita, wakiwemo maafisa watatu wa polisi, kwa mauaji ya Albert Ojwang.

Ojwang mwenye umri wa miaka 31, alifikwa na umauti katika mahabusu ya polisi alikokuwa anazuiliwa Juni 8 mwaka huu, siku moja baada ya kukamatwa kwa kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii akimtuhumu naibu mkuu wa polisi wa taifa hilo, Eliud Lagat, kwa ufisadi.

Albert Ojwang

Miongoni mwa maafisa watatu wanaokabiliwa na mashtaka ni kamanda wa kituo alichozuiliwa Albert Ojwang, huku fundi anayeshukiwa kufuta video za uchunguzi za CCTV katika kituo hicho cha polisi pia anakabiliwa na mashitaka.

Hata hivyo, Eliud Lagat, naibu mkuu wa polisi ya Kenya aliyehusishwa na mwathiriwa katika machapisho yake na ambaye ndiye aliyechochea kukamatwa kwake, si miongoni mwa washtakiwa waliotajwa na upande wa mashtaka.

Naibu mkuu wa polisi ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji, kulingana na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, siku chache baada ya tukio hilo, alitangaza kuwa anajitenga na majukumu yake wakati uchunguzi ukianza, hatua ambayo Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya iliona haitoshi.

Kulingana na Tume, Eliud Lagat ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji ya Albert Ojwang na anapaswa kujiuzulu kabisa kwenye wadhifa wake, akamatwe na afunguliwa mashtaka.

Kifo cha Albert Ojwang akiwa kizuizini kilizua msururu wa maandamano kote nchini Kenya na miito mingi ya kumtaka Eliud Lagat ajiuzulu, huku uchunguzi wake wa maiti uliokinzana na madai ya polisi kuwa mwathiriwa alijitoa uhai ukizua hisia kali.

Akihojiwa na maseneta wa Kenya, Douglas Kanja, mkuu wa polisi wa Kenya, alikiri kwamba ulikuwa uongo kabla ya kuomba radhi kwa umma.

Leave a Reply