You are currently viewing Prof. Janabi bosi mpya WHO- Afrika akichukua nafasi ya Dk. Ndugulile

Prof. Janabi bosi mpya WHO- Afrika akichukua nafasi ya Dk. Ndugulile

NA MWANDISHI WETU, GENEVA

Kikao Maalum cha Pili cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO kilichofanyika leo Jumapili, Mei 18, 2025 kimemchagua Profesa Mohamed Janabi kuwa  Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Profesa Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mshauri wa Rais wa Tanzania katika masuala ya afya na lishe, alikuwa anawania nafasi hiyo iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Dk Faustine Ndugulile kilichotokea Novemba 21, 2024.

Prof Janabi katika sera zake alikuwa ananadi uzoefu alionao katika sekta ya afya, ushauri kwa jamii, uongozi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na uwezo wa kuvutia ufadhili na mikopo nafuu katika sekta ya afya.

Prof. Janabi alikuwa miongoni mwa wagombea watano, ambao majina yao yaliingia katika mchakato wa uchaguzi Mei 18, mwaka huu.

Aidha Prof. Janabi alikuwa mgombea pekee kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, huku wagombea wanne walikuwa wakiwakilisha nchi za Afrika Magharibi ambao ni Dk. N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast,) Dk. Dramé Mohammed Lamine (Guinea,) Dk. Boureima Hama Sambo (Niger,) na Pr. Mijiyawa Moustafa aliwakilisha Togo.

Leave a Reply