Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameitaja Tanzania kuwa lango muhimu linalounganisha Afrika Mashariki na masoko ya dunia, akisisitiza kuwa nafasi ya nchi hiyo inaendelea kuwa ya kimkakati katika mfumo mpya wa uchumi wa dunia.
Akizungumza Juni 5 katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) 2026, Putin amesema Tanzania ina nafasi inayofanana na ile ya Uzbekistan katika Asia ya Kati, kwa kuwa ni kiungo muhimu kinachounganisha uchumi wa kikanda na vituo vikubwa vya biashara duniani.
“Tanzania ina nafasi kama hiyo katika Afrika Mashariki,” amesema Putin wakati akizungumzia nchi ambazo nafasi zao za kijiografia na uhusiano wao wa kiuchumi zinazozifanya kuwa madaraja muhimu yanayounganisha maeneo mbalimbali ya dunia.
Ameeleza mataifa yanayoweza kuoanisha maendeleo yao ya ndani na mahusiano imara na vituo vipya vya ukuaji wa uchumi duniani yanazidi kuwa na umuhimu mkubwa kadiri mifumo ya biashara ya kimataifa inavyoendelea kubadilika.
Putin pia amegusia kile alichokitaja kuwa ni mabadiliko yanayoendelea katika mfumo wa biashara ya dunia, akisema biashara ya kimataifa inajiondoa katika misingi yake ya awali iliyowekwa chini ya Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Kauli hizo zinakuja wakati Tanzania ikiendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya usafirishaji, maendeleo ya bandari na kuimarisha mtandao wa biashara wa kikanda, hatua zinazozidi kuimarisha nafasi yake kama lango kuu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
